Madaktari Bingwa Kutoka China Watua Moi


Madaktari Bingwa watatu wa upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (Neurosurgeon) kutoka hospitali ya kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking cha nchini China wamepokelewa MOI ambapo wataendesha mafunzo ya nadharia  na kuendesha kambi ya upasuaji siku ya jumatatu tarehe 25/02/2019.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MOI Profesa Charles Mkonyi amesema ujio wa madaktari bingwa hawa umewezekana kufuatia maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhakikisha Hospitali ya MOI na Chuo kikuu MUHAS zinaingia mkataba wa ushirikinao na Hospitali ya Peking jambo ambalo limetekelezwa chini ya Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto inayoongozwa na Mh. Ummy Mwalimu.

Katika utekelezaji huo, Taasisi ya MOI na Peking ziliingia mkataba wa ushirikiano katika maeneo ya tiba, utafiti na mafunzo.

Mkataba huo ulisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface pamoja na Rais wa Peking Profesa. Hongxia Yu ambapo MOI inanufaika katika kuboresha huduma za kibingwa za daraja la juu (Super specialised services) katika maeneo ya upasuaji wa Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema ujio wao utasaidia kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kwa kuwapa mbinu mpya za upasuaji na hivyo watanzania kupata huduma bora na za kibingwa za Mifupa, Ubongo,Mgongo na Mishipa ya Fahamu bila kwenda nje ya nchi.

“Tunamshukuru sana Mh Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuletea wataalamu hawa, Hospitali yetu ya MOI itanufaika sana kwani wenzetu hawa wana uzoefu mkubwa katika utoaji wa huduma hususani hizi ambazo tunatoa hapa MOI, binafsi nilifanikiwa kuiona hospitali yao kwakweli ni ya viwango vya kimatifa, sisi pia tunatamani kufikia viwango hivyo” alisema Dkt. Boniface.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Profesa Lawrence Mseru amesema ushirikiano huu utakuwa wenye manufaa makubwa kwa Watanzania kwani Hospitali ya Peking ni bora kutokana na uzoefu wa wataalamu wake pamoja na miundo mbinu ya kisasa  hivyo kufanya huduma zake kuwa bora.

“Mwaka jana mimi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI tulipata fursa ya kutembelea hospitali hii ya Peking, kwa kweli ni Hospitali kubwa ,nzuri na yenye huduma bora sana, naamini kupitia ushirikiano huu watashirikiana nasi kuboresha huduma hapa nchini” alisema Prof. Museru.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad