Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo jana wilayani Kaliua katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kolimba ambapo ameeleza kuwa idadi ya mimba za utotoni imeongezeka kutoka 21,889 mwaka 2017 hadi mimba 27,390 mwaka 2018.
Alisema kasi ya uwepo wa mimba za utotoni ni kubwa na haikubali na kutaka viongozi mkoani Tabora kubadilisha hali hiyo na kuwataka wazazi wajitahidi kuwalinda watoto wao.
Makamu wa Rais alieleza kuwa wakati mwingine wazazi hawajitokezi kutoa ushahidi pale inapojulikana watoto wao wamepata ujauzito na kwamba na kuongeza kuwa vitendo hivyo ni kuwakatili maisha yao.
Alisema kuwa hatua za makusudi zisipochukuliwa kuna uwezekano wa kuwa na wataalamu wa kike wachache kwa sababu ya kushindwa kutimiza ndoto zao.
Makamu wa Rais alipongeza maandamano yaliyofanywa mkoani Tabora katika kukemea na kudhibiti mimba za utotoni akisema anatambua jitihada zinazofanywa na mkoa kudhibiti hali hiyo, huku akiagiza jitihada zaidi ziongezwe kwa vile kuna ongezeko kubwa la mimba za utotoni mkoani Tabora.