Mapya Yaibuka Kilichomuua Godzilla

Mapya Yaibuka Kilichomuua Godzilla
DAR ES SALAAM: Licha ya dada wa aliyekuwa mwanamuziki wa Hip Hop Bongo, Golden Jacob Mbunda ‘Godzilla’, Joyce Mbunda kueleza kilichosababisha kifo cha staa huyo, bado kilichochukua uhai wake kimeibua mapya, Ijumaa limedokezwa. 



Godzilla alifariki dunia juzi Jumatano ya Februari 13, mwaka huu, nyumbani kwa wazazi wake, Mbezi-Salasala jijini Dar baada ya kuteswa na kitu kilichokwama tumboni kwa zaidi ya siku tatu na kumfanya atapike mfululizo. Mbali na hilo, pia ilifahamika kuwa jamaa huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari, lakini zaidi zaidi ni presha.



Kwa mujibu wa Joyce aliyezungumza na Gazeti la Ijumaa lililofika nyumbani hapo juzi, mwanamuziki huyo alikuwa akitapika kwa siku tatu mfululizo kabla ya kukata roho. Alisema rapa huyo aliyewahi kutamba na Wimbo la Lakuchumpa alianza kujisikia vibaya na alipokwenda hospitali ilibainika kuwa na malaria, sukari kuwa juu na presha.



“Jumapili (Februari 10, 2019) alilala muda mrefu, haikuwa kawaida yake. Baadaye aliomba barafu, tulivyompa akaanza kutapika ndipo tulipompeleka hospitalini na kugundulika ana malaria, sukari imepanda sana na presha imeshuka,” alisema Joyce kwa uchungu. “Pia kaka alisema kuna kitu kiling’ang’ania tumboni kama vile kinataka kutoka ila kinagoma, alijaribu kukitoa kwa kujitapisha, lakini hakikutoka.”



APATA NAFUU

Pamoja na kupata nafuu baada ya matibabu alilalamika kitu hicho kuendelea kukwama tumboni. “Alipewa ruhusa ingawa alikuwa anaendelea kutapika. Usiku alianza kuishiwa nguvu. Tukamrudisha hospitalini, akawekewa dripu mwisho akaandikiwa dozi ya siku 10. “Alipofika nyumbani alisali kabla ya kuingia kulala, lakini haikuchukua dakika 10 akaanza kuniita,” alisema Joyce na kuongeza:



“Nilimfuata chumbani nikiwa na mama, akatuambia anaona watu wengi wanamfuata, wamezunguka nyumba wanataka kumchukua. Akainuka ghafla akasema acha nitoke nje, tukamshika maana alikuwa anahangaika, akamlalia mama na hakuinuka tena.”



MAPYA SASA

Kufuatia kifo cha Godzilla, mapya yameibuka kiasi cha kuhusishwa na stress za muziki wake aliokuwa akiufanya kwa miaka mingi ambao haukumpa mafanikio aliyoyatarajia. Yapo madai kutoka kwa watu wa karibu na Godzilla kuwa jamaa huyo aliingia kwenye msongo kutokana na kazi yake ya muziki kuyumba na kukosa sapoti kama ilivyokuwa kwa baadhi ya wasanii wengine wa Hip Hop Bongo waliotangulia mbele ya haki.



KUTOONA MATUNDA

“Unajua kwa muda mrefu Godzilla alikosa sapoti kwenye muziki wake. “Jambo hili lilimsababisha kuwa kwenye msongo kwa kuwa tayari jina lake lilikuwa kubwa, lakini hakuwa anaona matunda ya kazi yake.



KAMA KINA NGWEA

“Na jambo hili siyo kwa Godzilla tu, kama utakumbuka wanamuziki kama Ngwea, Langa, Jize Mabovu, Mez B na wengine waliotangulia mbele ya haki, wengi walielezwa magonjwa yaliyowaua, lakini pia vifo vyao vilichangiwa na msongo.



STRESS ZA HATARI

“Ni sawa Godzilla inawezekana amekufa kwa kisukari au presha, lakini nyuma ya magonjwa hayo kuna stress za hatari ambazo alipitia. “Pia hali hii haikumtokea Godzilla tu, bali inawakumba wasanii wengi hasa kazi zao za sanaa zinaposhindwa kukidhi ndoto zao,” alisema mmoja wa watu wa karibu wa Godzilla aliyeomba hifadhi ya jina kwa kuwa si msemaji wa staa huyo.



TATIZO LA SONONA

Kwa mujibu wa mtaalam wa saikolojia aliyezungumza na Gazeti la Ijumaa, Dk Chris Mauki ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wasanii na hata watu wengi wanakabiliwa na tatizo la sonona (depression). Alisema sonona ni ugonjwa wa kisaikolojia usio na dalili za haraka zinazotambulika kwa nje unaomfanya mtu kutojitambua, kuvua nguo, kula jalalani, kuokota makopo, kuzungumza na kucheka wenyewe.



DALILI ZA SONONA

Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kukosa raha, kushindwa kushiriki mambo ya kufurahisha, kupoteza uwezo wa kufurahia jambo, kukata tamaa, kujiona mwenye hatia, kukosa matumaini ya siku zijazo na kupata magunjwa yasiyoambukiza kama presha.

Dalili nyingine ni mgonjwa kujiona hajafanya kitu cha maana, kujiona si wa maana na hana heshima. “Mtu anaweza kuwa na ugonjwa wowote, lakini chanzo cha magonjwa mengi yanayosumbua na kuua watu wengi nchini kwa sasa ni sonona,” alisema mtaalam huyo.



WASANII WAFANYE NINI?

Alisema ugonjwa au hali hiyo haitibiwi kwa kumeza kidonge kwani matibabu yake ni ya kisaikolojia zaidi. “Hakuna kidonge cha kubadilisha haiba ya mtu. Haiba ni jinsi mtu alivyozaliwa tangu akiwa mdogo,” alisema na kuongeza: “Cha msingi mtu asiweke malengo ambayo hawezi kuyafikia, ajifunze kukubali changamoto, kufanya uamuzi pale panapopaswa, kuwa na mipango, kutokuweka jambo linalokusumbua moyoni na kujali mno mwili wako.”



MASTAA WAMLILIA

Baadhi ya mastaa Bongo wameendelea kumlilia Godzilla kama ifuatavyo;

MWASITI ALMASI: Ooh God umetangulia Zizi (Godzilla) jamani! Niko kwenye maumivu makali mno! Mwenyezi Mungu naomba akupumzishe kwa amani kwenye nyumba yako ya milele.

FID Q: Inna lillah wainna ilaih raajiuun..Rest well young king!



Lulu Diva: Zilla (Godzilla) wewe jamani, huwezi kunifanyia hivi…Dah jamani Innalilah wainna lillah Rajiun.

SONGA: Mungu akulaze pema King Zillah (Golden Jacob), kama alivyo samaki na mengi ya kusema ila mdomo una maji. Umetuachia huzuni kubwa.

KALA JEREMIAH: Pumzika kwa amani ndugu, hakika umetuachia maumivu makali. Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwa.

Vanessa Mdee: Rest easy King. Happy we lived to witness your greatness. May your legacy live on.

Dully Sykes: Nasikitika kupata taarifa za msiba wa mdogo wangu. R.I.P Zilla!

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad