Hatua ya Marekani ya kuwawekea vikwazo vya usafiri maafisa wakuu wa tume ya uchaguzi pamoja na viongozi wengine nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya DRC imeendelea kuzua hisia mbalimbali.
Serikali ya Marekani ilichukua hatua hiyo mwishoni mwa wiki kwa madai kwamba viongozi hao walijipatia utajiri kwa njia za rushwa.
Msemaji wa Tume huru ya uchaguzi Jean Pierre Kalamba, kupitia barua iliyotiwa saini na tume hiyo amekanusha tuhuma hizo za rushwa na kuongeza kuwa ilifanya kazi nzuri ya kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa njia ya amani.
Hali ambayo ilisaidia marais wawili wa Congo kupokezana madaraka kwa njia ya amani.
Bwana Kalamba ameahidi kutoa ripoti ya maandalizi ya uchaguzi kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka huu.
Kwa upande wake Lambert Mende ambaye alikuwa msemaji wa serikali ya Joseph Kabila amesema vikwazo hivyo havitakuwa na mafanikio yoyote.
''Marekani inasimama na watu wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kufuatia historia waliyoweka kwa kufanikisha mchakato wa viongozi kupokezana madaraka kwa amani. Uchaguzi ulionesha ari ya wakongo ya kutaka mabadiliko ya serikali na taasisi zinazowajibika. Hatahivyo, kuna madai kwamba hapakuwa na uwazi katika machakato wa uchaguzi.'' ilisema taarifa iliyotolewa na Marekani.
Viongozi waliyowekewa vikwazo ni pamoja na mwenyekiti wa tume ya huru ya uchaguzi ya Congo DRC (CENI), Corneille Nangaa, naibu wake Norbert Basengezi Katintima.
Marekani imewawekea vikwazo vya usafiri viongozi wa DRC
0
February 25, 2019
Tags