Mashamba ya Mo Dewji, Sumaye Yaibua Mjadala Mkubwa Bungeni

Mashamba ya Mo Dewji, Sumaye Yaibua Mjadala Bungeni
Serikali imesema mashamba sita yanayomilikiwa na mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’ yapo chini ya uangalizi na kama atashindwa kutekeleza masharti watayafuta.

Akijibu hoja za wabunge jana walizozitoa katika mjadala wa taarifa ya kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema awali mfanyabiashara huyo alipewa onyo katika mashamba 12 kati ya 21 aliyokuwa akimiliki.

Alisema Serikali tayari imefuta hati za mashamba sita bado sita ambayo yapo kwenye uangalizi na kubainisha kuwa Tanzania ina mashamba makubwa 2000 ya kilimo na ufugaji.

“Haijatokea nikapata agizo kutoka kwa Rais kuwa nifute hati ya shamba la mtu,”alisema Lukuvi.

Alisema zoezi hilo ni utatuzi wa kero zilizotolewa na wabunge baada ya kuwapa dodoso la kuandika kero zao.

Alisema asilimia 60 ya kero zilizoandikwa na wabunge zilihusiana na mashamba pori na migogoro ya ardhi.

Lukuvi alisema kwa kipindi cha miaka mitatu wamefuta mashamba 46 katika maeneo mbalimbali ambayo yameshindwa kutimiza masharti.

Alisema katika utafiti waliofanya wamebaini mashamba hayo yametumika kama rehani ambazo zimewawezesha kupata zaidi ya Sh1 trilioni.

Lukuvi alisema kiasi hicho cha fedha kimeenda kuwekezwa katika miradi mingine na si kilimo ambapo kama wangewekeza fedha zote kungekuwa na mabadiliko kwenye sekta hiyo.

“Mheshimiwa Msigwa (mbunge wa Iringa Mjini-Chadema) hakuna uhalali wa kuunda kamati kwa sababu mambo haya yamefanyika kwa kufuata sheria. Nendeni mkahangaike na majimbo yenu,” alisema Lukuvi.

Awali, Wabunge wa Upinzani na  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliingia katika mvutano na gumzo  kuhusu taratibu zilizotumika kuyafuta, huku Spika wa Bunge, Job Ndugai, akilazimika kuzima mjadala huo, akisema anadhani suala la  Sumaye liko mahakamani, hivyo si jambo jema kuendelea kulijadili bungeni.

Kabla ya Spika Ndugai kuzima mjadala huo usiendelee, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa, alisema haoni shida ya unyang’anywaji wa mashamba hayo, lakini taratibu zinazofanyika siyo sahihi.

Akichangia, Msigwa alisema pamoja na mambo mengine, kamati haikuweka baadhi ya mapendekezo yake katika taarifa ambayo ni kuitaka serikali kuunda kamati ya kuchunguza unyang’anywaji wa mashamba hayo.

Kutokana na kauli hiyo ya Msigwa, Mbunge wa Simanjiro (CCM), James Ole Millya,  alisimama na kuomba kumpa taarifa mzungumzaji huyo akisema: “Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mbunge, mimi natoka Jimbo la Simanjiro, takribani mwezi mmoja uliopita, Waziri alifuta mashamba zaidi ya 200 na nina hakika mashamba haya yote yalikuwa hayajafuata utaratibu na wala asipende kumchafua waziri.”

Alipomaliza kutoa taarifa hiyo, Msigwa alimshangaa Millya akisema: “Mimi nadhani unaenda haraka, mimi sijamchafua sasa ni wapi namchafua, nimezungumza, nimesema sina tatizo kabisa na mashamba makubwa kunyang’anywa kwa mujibu wa sheria na kufuatwa utaratibu.”

“Nimetoa mfano moja, Mheshimiwa Sumaye alikuwa na shamba lake, alilipata kihalali na ameliendeleza mpaka wanachukua shamba lake, alikuwa na ng’ombe 200 kwenye shamba lake, alikuwa na kondoo 350, nyumba kubwa ya umwagiliaji, kisima na ghala la mazao, anaambiwa hajaendeleza, mimi nasema unyang’anyaji huu siyo sahihi.”

Alisema anafahamu kwamba Rais kubadilisha hati, anayo mamlaka hiyo na kwamba mpaka sasa  ukiangalia hali ilivyo, ukiangalia akina Mo (Mohamed Dewji) wamenyanganywa mashamba yao ni lazima kamati ya uchunguzi iundwe ili kuangalia unyang’anywaji unavyoenda.

Suala hilo lilimwinua kitini Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga, na kutoa taarifa kwa mzungumzaji huyo kwamba kinachoonekana kupigiwa kelele ni shamba la Sumaye.

Mlingwa amesema: “Hapa linalopigiwa kelele ni suala la shamba la Mheshimiwa Sumaye, ambaye taarifa zake ni hizi, alikuwa na shamba la ekari 326, amekaa nalo miaka 15, ameendeleza ekari sita, amejenga kibanda kimoja kina watu watatu.

“Katika shamba la Sumaye, kulikuwa na miembe mitatu, miche ya mahindi 76, mnazi mmoja, ng’ombe watatu, mbuzi 11, bata sita na kuku tisa.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad