Mkurugenbzi wa Kampuni ya wawekezaji kutoka Falme ya Kiarabu ya Ortello Business Cooperation (OBC), Isack Mollel (59), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, akikabiliwa na mashtaka 10 ya kuajiri wafanyakazi 10 wa kigeni bila vibali vya kufanya kazi nchini.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Niku Mwakatobe, Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Idara ya Kazi, Emanuel Mweta, alisema mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo huku akijua ni kinyume cha sheria katika kipindi cha Novemba 2018 hadi Februari mwaka huu.
Upande wa utetezi katika shauri hilo la jinai, ulikuwa ukiwakilishwa na mawakili, Daudi Haraka, Method Kimomogoro na Goodluck Peter, ambapo inaelezwa baadhi ya wafanyakazi hao waliajiriwa kama mafundi magari, wapishi na madereva.
Aliwataja wafanyakazi hao raia wa kigeni walioajiriwa bila kufuata taratibu za sheria kuwa ni Darweshi Jumma, Riaz Aziz Khan, Mohammad Tayyab, Ali Bakhash, Abdulrahman Mohammed, Imtiaz Ahmad Fiaz, Zulfiqar Munin, Martin Crasta, Hamza Sharif na Arshad Mohammad.
Wiki iliyopita wafanyakazi hao walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ya kufanya kazi nchini pasipo kufuata sheria.
Jana baada ya Mollel kufikishwa mahakamani, Mwendesha Mashtaka huyo alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba Mahakama hiyo kuweka masharti magumu ya dhamana kwa mshtakiwa huyo kwani upatikanaji wake ni mgumu.
Alisema inatilia shaka uwepo wake hivyo mahakama iweke masharti magumu kwani awali walishindwa kujua alipo wakati wafanyakazi hao wanafikishwa mahakamani.
Wakili wa utetezi Haraka, alidai mahakamani hapo kuwa ombi hilo halina mashiko kwani awali mshtakiwa huyo hakupewa hati ya kuitwa mahakamani hapo hivyo hakujua kama anahitajika mahakamani na kwa kuwa shtaka hilo lina dhamana Mahakama impe dhamana kwa masharti nafuu.
Hakimu Mwakatobe alikubaliana na ombi hilo na kutoa masharti kwa mshtakiwa huyo kudhaminiwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja anasaini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh milioni 40 kila mmoja ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi itakapotajwa Februari 22, mwaka huu.
Mwishoni mwa wiki iliyopita wafanyakazi hao 10 wenye asili ya Asia wa kasri la mfalme wa Abu Dhabi inayosimamiwa na OBC iliyopo eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro, mkoani hapa, walipandishwa kizimbani kwa kosa la kufanyakazi nchini kinyume cha sheria za ajira kwa wageni.
Februari 22, mwaka huu Mkurugenzi huyo na wafanyakazi hao watafikishwa tena mahakamani hapo kesi zao zitakapotajwa.
Awali, Februari 13 mwaka huu, akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, aliagiza kukamatwa au kujisalimisha kituo cha polisi kwa Mkurugenzi huyo kwa tuhuma za kuwaajiri wafanyakazi hao bila kufuata utaratibu.
Alimwagiza Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Longinus Ribishumbwamu, kumsaka mkurugenzi huyo kabla hajamaliza ziara yake jijini Arusha, ambapo taarifa zinadai Mkurugenzi huyo alijisalimisha polisi jioni ya siku hiyo agizo hilo lilipotolewa.
Mkurugenzi anayesimamia kampuni ya Mfalme ya OBC apandishwa kizimbani
0
February 16, 2019
Tags