Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Itigi Kortini Tuhuma za Mauaji Kanisani

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Itigi Kortini Tuhuma za Mauaji Kanisani

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni, Pius Luhende (54) na maofisa sita wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida wakikabiliwa na kosa la mauaji ya Isack Petro.

Petro anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi akiwa kwenye Kanisa la Wasabato lililoko Kijiji cha Kaskazi wilayani Manyoni mkoani Singida Februari 2, mwaka huu.

Wakisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Consolata Singano, Wakili Mkuu wa Serikali, Michael Ng’oboko kwa kushirikiana na Wakili Emily Kiria, walidai Luhende na wenzake sita wanashtakiwa kwa kutenda kosa hilo Februari 2, mwaka huu, katika Kijiji cha Kaskazi wilayani Manyoni.

Washtakiwa wengine ni ofisa wanyamapori wa halmashauri hiyo, Rodney Ngalamba (42), askari wanyamapori wa Kijiji cha Doroto katika Hifadhi ya Rungwa, Makoye Stevin na Mwanasheria wa Halmashauri ya Itigi, Erick Paul (31).

Wengine ni Ofisa Tarafa ya Itigi, Eliuta Augustino (43), Ofisa Kilimo na Mifugo wa Halmashauri ya Itigi, Silvanus Lungwisha (50) na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kaskazi katika halmashauri hiyo, Yusuph John (25).

Ng'oboko alidai washtakiwa kwa pamoja walishirikiana kumuua kwa kumpiga risasi Isack Petro ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.

Wakili Kiria alidai mahakamani kuwa, washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume cha Sheria Kanuni ya Adhabu Kifungu cha 116 na 197.

Wakili Ng’oboko alidai mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, na kuomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe itakayopangwa.

Hakimu Singano aliwataka washtakiwa kutojibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri lao. Kesi hiyo ina hadhi ya kusikilizwa na Mahakama Kuu.

“Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza shauri lenu, hivyo naahirisha shauri hili hadi siku ya Februari 25, mwaka huu, kwa ajili ya kuja kutajwa, washtakiwa wote warudi mahabusu," alisema Hakimu Singano.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad