Mkuu wa Mkoa atajwa kwenye ufisadi wa Bilioni 3.5 Bungeni

Mkuu wa Mkoa atajwa kwenye ufisadi wa Bilioni 3.5 Bungeni
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Vedasto Ngombale amesema kuwa katika ukaguzi maalum katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2017 kamati yake imebaini kuwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Fatma Mwasa alitumia madaraka yake vibaya wakati wa Uongozi wake na kusababisha ubadhirifu wa Shilingi Bilioni 3.5.

Akiwasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati ya LAAC kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni, 2017, Mwenyekiti Vedasto Ngombale, alisema kamati hiyo iliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kufanya ukaguzi maalum kutokana na kutilia shaka taratibu zilizotumika katika kumpata mkandarasi Saram Co.Ltd katika zabuni za ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi na Kituo cha Afya.

Alisema ukaguzi huo umefanyika katika hesabu za kipindi cha kuanzia 2012/13 hadi 2016/17 na kubaini mambo mengi ambayo yamefanyika bila nidhamu ya usimamizi wa fedha za umma na ukiukwaji wa taratibu na kanuni zinazosimamia masuala ya fedha.

Alisema ukaguzi huo umebaini moja ya chanzo kikubwa cha ubadhirifu huo ni matumizi mabaya ya madaraka yaliyotumiwa na Mwasa katika miradi iliyotekelezwa na kampuni ya Saram Co.Ltd.

“Mkuu wa Mkoa wa wakati huo katika miradi iliyotekelezwa na kampuni ya Saram alitumia vibaya madaraka kwa kumwelekeza Mkurugenzi(Halmashauri ya Kaliua), Wenyeviti wa kamati za tathimini, Bodi ya zabuni na Mkuu wa Kitengo cha ununuzi kutoa zabuni kwa kampuni hiyo,” alisema.

Alibainisha kuwa Kampuni hiyo Mkurugenzi wake ni mtu aliyekuwa na mahusiano ya ndani na Mkuu wa Mkoa huyo wa wakati huo.

“Ukaguzi umebaini watumishi wawili tu wa kitengo cha manunuzi kati ya watumishi 66 wa halmashauri waliobainika kuhusika na ubadhirifu huo ndio wamechukuliwa hatua,” alisema.

Alisema ubadhirifu huo una sura ya kijinai ambapo malipo ya awali ya Sh. milioni 121.7 yaliyofanyika kwa kutumia nyaraka za dhamana toka Benki ya Equity na nyaraka hizo zilighushiwa na mkandarasi.

“Malipo ya awali ya Sh. milioni 51.6 hayakurejeshwa na mkandarasi na hivyo kusababisha hasara kwa Halmashauri na fedha Sh.milioni 11.3 alizolipwa mkandarasi ni zaidi ya thamani ya kazi zilizofanyika kwa mujibu wa mchanganuo wa gharama za kazi zilizotekelezwa,” alisema.

Aidha alisema malipo yaliyofanyika kwa mkandarasi bila kuonyesha vipimo vya kazi na mchanganuo wa kazi ambazo hazikufanyika katika mradi wa ujenzi wa jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD).

“Malipo ya Sh. milioni 44.7 yalifanyika mara mbili kwa mkandarasi kwa kazi zilizofanyika katika mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi, ”alisema.

Ngombale alisema udanganyifu wa Sh. milioni 178 katika ununuzi na hati za malipo na kutozingatia masharti ya sheria za ununuzi.

“Pia malipo ya mkandarasi kwa kazi za mfuko wa barabara kwa kazi ambazo hazikufanyika kiasi cha Sh.milioni 31.6 na malipo yalipo Sh.milioni 393.6 yaliyofanyika katika akaunti ya Amana ambayo hatima zake hazijawasilishwa kwa ukaguzi,” alisema.

Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa matumizi ya kiasi cha Sh.Milioni 78.5 yenye mashaka kwa ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa maabara na usimamizi dhaifu katika ukusanyaji wa ushuru wa tumbaku uliopelekea kutokukusanya mapato ya zaidi ya Sh. bilioni 1.35.

“Malipo mbalimbali yenye viashiria vya ubadhirifu na kughushi nyaraka yenye kiasi cha Sh.bilioni 1.02,”alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad