WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amepiga marufuku makongamano ya wafugaji yenye lengo la kumpongeza Rais Dk John Magufuli kwa uamuzi aliochukua wa kuwasaidia badala yake ametaka watumie kipindi hiki kifupi walichopewa kuanisha maeneo ambayo yamepoteza sifa za uhifadhi yaweze kuchukuliwa kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Hivyo ametaka wafugaji kote nchini kujipanga na kupendekeza maeneo yaliyopoteza sifa za uhifadhi, mashamba yasiyoendelezwa ili wafugaji waweze kuyapata kwa ajili ya malisho ya mifugo yao kama sehemu ya kuunga mkono uamuzi uliotolewa wa kusaidia sekta hiyo.
Akizungumza katika mkutano wa kuwasilikiza wananchi waishio kando ya Hifadhi ya Pori la Akiba la Maswa wilayani Meatu mkoani Simiyu kwenye ziara ya Kamati ya mawaziri nane, Waziri Mpina alisema tangu mwaka 2000 tume zaidi ya 27 ziliundwa na Bunge na Serikali kushughulikia migogoro zaidi ya 1,095 lakini asilimia 99 ya mapendekezo ya tume hizo hayajatelezwa hadi leo.
Mpina alisema tume nyingi zilizoundwa miaka ya nyuma kushughulikia migogoro hiyo zilichakachuliwa hata kabla ya kukabidhi matokeo ya mambo waliyobaini kwa kuwa kwenye migogoro hiyo wako baadhi ya viongozi wa Serikali wako nyuma wana manufaa binafsi wanayopata ndio maana mapendekezo yaliyotolewa ya kutatua migogoro hiyo hayajawahi kutekelezwa hadi leo.
Alisema baadhi ya watendaji wa Serikali walilazimika hata kutoa rushwa ili kubadilisha maamuzi ya tume zilizokuwa zinaundwa kushughulikia migogoro hiyo kwa sababu wananufaika na migogoro hiyo.
“Mhe John Pombe Magufuli akasema hapana nitaunda tume ambayo haitapokea rushwa timu ya Lukuvi mnaiona ina sura ya kupokea rushwa? Vichwa vya kina Mpina unaweza ukawapa nini wakakubali, akasema wananchi wangu watahangaika mpaka lini, watauana mpaka lini mifugo mingi imedhulumiwa kwa kivuli cha uhifadhi, Mhe Rais akasema nitaunda tume ndio hii sasa ya mawaziri 8”alisema Mpina
Mpina aliwahakikishia wananchi kuwa mapendekezo yaliyotolewa na wananchi yatafika kwa Rais tofauti na tume zingine zilizotangulia zilikuwa hazina uwazi wa namna ya kuchukua maoni na namna ya kufikisha mapendekezo serikalini.
“Mhe Rais akasema nitaunda timu ambayo itaandaa waraka wa baraza la mawaziri ili waraka ule uamuliwe na Serikali hapo ndipo utaona huyo ndio Dk John Pombe Joseph Magufuli ambaye amejipambanua katika kuhakikisha kwamba matatizo ya wananchi yanashughulikiwa na yanamalizika”alisema Mpina
Kufuatia hali hiyo Waziri Mpina ameagiza wafugaji wote nchini kusitisha makongamano na maandamano ya kumpongeza Rais kwa sasa kwani Rais amewapa kazi wakulima, wafugaji, wavuvi kuangalia maeneo ambayo yamepoteza sifa yaweze kupendekezwa ili wafugaji wayapate.
“Sisi kama wafugaji tusipoteze muda wa makongamano na kumshangilia Mhe Rais wakati ametupa kazi kubwa ya kupendekeza maeneo hayo ili mwisho tuyapate, yafutwe tuweze kufanya shughuli kilimo, ufugaji”alisema
Hivyo Waziri Mpina amekataa kuhudhuria makongamano ya vyama vya wafugaji ambao wamemualika kuhudhuria sherehe hizo na kuwataka kujipanga vizuri kupendekeza ili kuitumia vizuri nafasi ya pekee waliyopewa na Rais Dk Magufuli.
“Hakuna kiongozi mwingine yoyote katika historia ya Tanzania ambaye amekuwa na mtizamo wa kutatua kero za wananchi wake kama Mhe Dk John Pombe Magufuli, Rais huyu historia itaandika ya Tanzania na hata ya dunia kwa mtazamo wake ambapo wananchi wengi wakitaka kupaza sauti zao wanazuiwa na watu wachache ambao walikuwa na masilahi katika mambo hayo sasa hayo yote yamefika mwisho”alisisitiza Waziri Mpina.
Akiwasilisha maelezo na mapendekezo ya wananchi waishio Kando ya Pori la Akiba la Maswa mmoja wa wananchi hao, Deus Martin alisema hadi sasa jumla ng’ombe 75 wanashikiliwa katika Kituo cha Buturi kwa zaidi ya mwaka mmoja na miezi 4 bila kuachiwa na kurudishiwa wenyewe.
Alisema mpaka uliopo sasa uliwekwa mwaka 1984 bila kuwashirikisha wananchi ambapo katika kipindi hicho wananchi walikuwa wanaishi zaidi ya kilomita 10 kutoka mpaka uliowekwa sasa hivyo wananchi walihamishwa kwa nguvu na kusababisha ukosefu wa malisho hadi sasa.
Hivyo wameomba kupewa maeneo hayo waliyoyaacha ndani ya hifadhi ili wayatumie kwa ajili ya malisho kwa kipindi cha kuanzia Novemba hadi Juni.Pia wameomba Sheria ya kuwazuia ndani ya mita 60 kutoka kwenye kingo za mito ifutwe ili waweze kutumia maeneo hayo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Maalum na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwahakikishia wananchi walioondolewa kupisha mita 500 warudi waendelee na shughuli zao kwani Rais Dk John Magufuli alishasitisha zoezi la kuwaondoa wananchi hao.
Lukuvi aliwahakikishia wananchi waishio pori la Akiba la Maswa kuwa mapendekezo waliyotoa ya kuomba kuongezewa eneo la malisho wamechukua na watayasilisha kwa Rais kama yalivyo kwa uamuzi zaidi.
Mawaziri wanaounda timu hiyo mbali na Mpina na Lukuvi ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Suleiman Jafo, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamish Kigwangala, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Mussa Sima.
Mpina Agoma Kuhudhuria Makongamano Ya Vyama Vya Wafugaji....Asisitiza wafanye kazi waliyopewa na Mheshimiwa Rais
0
February 23, 2019
Tags