Msichana Aliyejiunga na Islamic State Kupokonywa Uraia wa Uingereza

Msichana Aliyejiunga na Islamic State Kupokonywa Uraia wa Uingereza
Shamima Begum, aliyejiunga na kundi la wapiganaji wa Islamic State nchini Syria akiwa na miaka 15, atapoteza uraia wake Uingereza.

Duru kutoka serikalini zilisema inawezekana kumvua uraia msichana huyo mwenye umri wa miaka 19 raia wa Uingereza kwasababu ana nafasi ya kupata uraia wa nchi nyingine.

Wakili wa familia yake, Tasnime Akunjee, amesema "wamesikitishwa" kwa uamuzi huo na wanatathmini 'njia zote kisheria' kukabiliana na hatua hiyo.

Begum, aliyeondoka London mnamo 2015, alisema anataka kurudi nyumbani.

Alipatikana katika kambi ya wakimbizi nchini Syria wiki iliyopita baada ya kuondoka Baghuz, inaarifiwa - ngome ya wapiganaji wa IS - na kwamba alijifungua mtoto wa kiume mwishoni mwa juma.

Katika mahojiano na BBC Jumatatu, Begum amesema hakutaka kuwa 'sura ya wasichana' wa IS na kwamba anachotaka sasa ni kumlea mtoto wake kwa umakini nchini Uingereza.

ITV News ilipata barua aliotumiwa mamake Begum, ikimtaka amueleze binti yake kuhusu uamuzi huo.

Uhusiano na Bangladesh

Kwa mujibu wa sheria nchini Uingereza mtu anaweza kupokonywa uraia iwapo waziri wa mambo ya ndani ametosheka kwamba ni kwa 'maslahi ya wema kwa umma' na kwamba baada ya hatua hiyo hawatokosa uraia katika nchi nyingine.

Begum amesema alisafiri kwenda Syria akitumia pasipoti ya dadake ya Uingereza, lakini alipokonywa alipovuka mpaka.

Inaaminika ana asili ya Bangladeshi lakini alipoulizwa na BBC, ameeleza kwamba hana pasipoti ya Bangladesh na kwamba hajawahi kwenda katika nchi hiyo.

Lakini vipi kuhusu mwanawe aliyemzaa? mtoto aliyezaliwa na mzazi aliye na uraia wa Uingereza kabla ya kupokonywa uraia, bado anatizamwa kuwa raia wa Uingereza.

Wakati inawezekana kimsingi kumpokonya mtoto uraia , maafisa watahitaji kupima sawa haki zao dhidi ya tishio walilonalo.

Islamic State limepoteza sehemu kubwa ya maeneo ambayo yalidhibiti , lakini kati ya wapiganaji 1000 na 1500 inaaminika wamesalia katika eneo la kilomita 50 kwa mraba karibu na mpaka wa Syria na Iraq.

Mwaka jana, wanaume wawili raia wa Uingereza, waliotuhumiwa kuwa wafuasi wa mtandao wa IS unaojiita "The Beatles" walipokonywa uraia baada ya kukamatwa Syria.

'Kulipiza kisasi'

Begum amesema hajutii kusafiri kwenda Syria, hatahivyo, amesema hakubaliana na kila kitu ambacho kundi hilo la IS limefanya.

Ameiambia BBC kwamba "ameshangazwa" na shambulio la 2017 katika ukumbi wa Manchester Arena - lilisobabisha vifo vya watu 22 na ambalo kundi hilo la IS lilikiri kutekeleza - lakini pia alifananisha shambulio hilo na mashambulio ya kijeshi katika ngome za IS akieleza kwamba ni "kulipiza kisasi".

Begum aliondoka Uingereza na rafiki zake wawili wa shule, Kadiza Sultana na Amira Abase mnamo Februari 2015. Inadhaniwa huenda Sultana alifariki wakati nyumba moja ililipuliwa, na Abase hajulikani aliko.

Begum amezaa mtoto wa kiume mwishoni mwa juma baada ya kupoteza watoto wengine wawili, waliofariki.

Mumewe, raia wa Uholanzi ambaye amesilimu, inadhaniwa amejisalimisha kwa wapiganaji wa Syria wiki mbili zilizopita.

Begum ana haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa kumpokonya uraia Uingereza.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad