Mwanaume mmoja katika Kaunti ya Kakamega nchini Kenya amenusurika kifo masaa machache baada ya wawili hao kugombana sababu ikiwa ni mkewe kukataa kumpikia ugali.
Tukio hilo limedaiwa kutokea Jumapili katika kijiji cha Emukaba kilichopo Kaunti hiyo ya Kakamega, ambapo Inadaiwa kuwa mwanaume huyo alimvamia mkewe na kumjeruhi sehemu mbalimbali kwa kisu na kisha mwenyewe kumeza vitu vilivyosadikika kuwa na sumu hadi alipokutwa na majirani na kupelekwa hospitali.
Baada ya kumjeruhi mkewe, mwanaume huyo alimwosha mkewe kwa maji na kumfunika kwa blanketi ili kuficha tukio alilolifanya, lakini majirani waliotembelea nyumbani kwake walikuta mwanamke huyo akiwa amefichwa ndani.
Mshauri Mkuu wa masuala ya kijamii na kijinsia, Peninah Mukabane ambaye alitembelea kijijini hapo amesema, "Tunashuhudia ugomvi wa watu wengi majumbani kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya na kutokuwa na uwezo wa kuzikabili changamoto za kifamilia zinazowakabili".
Naye Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi (ODCP) wa Kaunti ya Kakamega, Joseph Chebii amesema kuwa, "Mtuhumiwa alijaribu kujiua mwenyewe kwa kumeza vitu vilivyosadikika kuwa na sumu na alikimbizwa hospitali kwa matibabu".
Hata hivyo kwa mujibu wa ODCP Chebii, mwanaume huyo alifariki akiwa hospitalini na mwili wake kupelekwa mochwari, huku akisema polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.