Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki ameeleza kuwa anafuatilia taarifa juu ya madai ya kupotea Mwenyekiti wa Kijiji cha Gijedubung anayetokana na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye anafahamika kwa jina la Faustine Kwaslema.
Kwa mujibu wa Kamanda Nsimeki, kwa sasa hana taarifa ya awali juu ya tukio hilo bali ameanza kulifuatilia ili kujua nini kilichotokea kwa mwenyekiti huyo ambaye inasemekana amepotea kusikojulikana mpaka sasa.
"Ngoja nifuatilie maana sijaipata bado kama mtu ametoweka vyombo vipo, wenye ndugu zao walitakiwa wapeleke taarifa polisi, ila na wao wanafanya makosa makubwa msemaji ni mimi nashangaa kwanini wao wanazungumza", amesema Kamanda Nsimeki.
Mapema leo kupitia mitandao ya kijamii kulianza kusambaa taarifa ya juu ya hali ya hofu na wasiwasi kufuatia kutoonekana kwa Mwenyekiti huyo wa Kijiji.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa ilimnukuu Mtendaji wa Kijiji, John Isdory ambaye amedai Faustine alitoka nyumbani kwake asubuhi ya Februari 9 akiwa na usafiri wa Pikipiki na hakurejea tena mpaka sasa.