WAKATI homa ya mechi ya kimataifa ya mabingwa Afrika kati ya Simba na Al Ahly ikizidi kupamba moto, imebainika kuwa mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi ndiye mchezaji anayewapasua vichwa vilivyo viongozi wa benchi la ufundi la Waarabu hao.
Hiyo ni kutokana na rekodi nzuri aliyonayo dhidi ya timu za Waarabu ambapo kila anapokutana nao uwanjani mara nyingi amekuwa akiwasumbua.
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Haruna Niyonzima ameliambia Championi Ijumaa kuwa mara tu baada ya kufika Misri walipata taarifa kuwa Okwi ndiye anayewaogopesha zaidi Waarabu hao na tayari beki wa zamani wa TP Mazembe ya DR Congo, Mmali, Salif Coulibaly ambaye anawatumikia Waarabu hao kwa sasa, amepatiwa jukumu la kumdhibiti.
“Hiyo ndiyo taarifa mpya ambayo tumeipata hivi karibuni, lakini tunaendelea vizuri na maandalizi yetu na katika mechi hiyo ya Jumamosi tutapambana vilivyo kuhakikisha tunafanya vizuri.
“Kwetu sisi tunahitaji ushindi katika mchezo huo na kama siyo ushindi basi sare lakini siyo kupoteza mchezo huo, kwa hiyo pamoja na kumwekea ulinzi mkali Okwi lakini bado naamini tutafanya vizuri tu,” alisema Niyonzima.