Oman yajivunia uwekezaji Z'bar

Oman yajivunia uwekezaji Z'bar
Mwakilishi wa Kampuni ya Arabian Industries ya Oman, Sheikh Amor Al –Suleimani, amesema Oman inajivunia kuona wawekezaji wa taasisi na kampuni za kibiashara kutoka nchi hiyo, wanashawishika kuongeza kasi ya uwekezaji kwenye miradi ya utalii na uvuvi wa Bahari Kuu.

Mwakilishi huyo ameyasema hayo Chukwani mwishoni mwa wiki alipozungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na kusema kuwa anaamini uwekezaji huo utaongeza mapato na kuimarisha uchumi wa nchi hizo mbili.

Al – Suleimani alimweleza Balozi Iddi kuwa, wananchi wa Zanzibar na Oman hawana sababu ya kutoshirikiana kutokana na uhusiano wao wa kihistoria.

Alisema uongozi wa Arabian Industries tayari umeshawishika kuwekeza katika miradi ya sekta ya utalii kwa kujenga hoteli ya nyota tano kutokana na fursa za uwekezaji zilizoko visiwani Zanzibar.

Akitoa shukrani zake kwa ujio wa ujumbe huo wa Arabian Industries, Balozi Iddi alisema Zanzibar imezungukwa na samaki kutokana na kuwa na bahari pembe zake zote inayotoa fursa kwa wawekezaji wa nje kuanzisha miradi yao ya uvuvi wa Bahari Kuu.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (Zipa) iko tayari kushirikiana na taasisi au kampuni itayojitokeza kuwekeza kwenye sekta hiyo yenye uwezo wa kutoa ajira nyingi kwa wazawa ili kupunguza ukali wa maisha.

Balozi Iddi pia alikutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro, aliyefika Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Dk. Damas Ndumbaro alisema anatambua umuhimu wa Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo bado ana safari ndefu ya kujifunza mambo mengi kutoka kwa watangulizi wake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad