Mikoa yote nchini imeanza operesheni kali dhidi ya waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi kwa sababu wamekuwa chanzo cha mauaji ya watu nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro jana katika Kijiji cha Nyamilangano Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri hiyo pamoja na Viongozi wengine wa Wilaya hiyo.
Alisema Jeshi la Polisi halina ugomvi na waganga wa jadi, bali linawatafuta wale wanaojihusisha na kupiga ramli chonganishi wanaohusishwa na vitendo vya mauaji.
Pia amesema hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari kwa kuwa tayari wamefanikiwa kuanza kudhibiti mauaji ya watoto katika mikoa ya Njombe na Simiyu.
Sirro alisema Jeshi la Polisi lilifanikiwa kudhibiti na kukomesha mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino, lakini kwa sasa yameanza kujitokeza mauaji ya watoto ambayo yanatokana na uchonganishi wa waganga wa jadi.
IGP alisema ni lazima wawasake na kuwachukulia hatua kali na kwamba suala la kupiga ramli chonganishi ni ushamba ambao umepitwa na wakati.