Patrick Aussems ajitetea na kipigo cha Al Ahly

Patrick Aussems ajitetea na kipigo cha Al Ahly
Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Patrick Aussems ametolea maelezo juu ya kipigo cha pili ilichokipata timu yake kutoka kwa Al Ahly ya nchini Misri, Jumamosi iliyopita pamoja na mikakati yake kama kocha katika michezo iliyobaki.

Akizungumza mara baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa JNIA jioni ya leo, Aussems amesema kuwa wameona utofauti mkubwa kati ya Al Ahly, AS Vita Club na klabu yao na hilo limewajenga katika kuwekeza zaidi ili kupata matokeo mazuri ya michezo ya  nyumbani.

"Malengo yetu sasa ni kushinda michezo yetu yote ya nyumbani, mimi na uongozi tulifahamu mapema kuwa mchezo dhidi ya Al Ahly na AS Vita Club itakuwa migumu na ndicho kilichotokea", amesema.

"Tupo bado kwenye michuano na michezo mitatu imebakia, tumemfunga JS Saoura na wao baada ya hapo wametoa sare mechi mbili, kwahiyo kila kitu kinawezekana", ameongeza.

Pia amesema kuwa moja ya malengo aliyojiwekea pamoja na uongozi wa klabu wakati michuano ya Klabu Bingwa Afrika inaanza ilikuwa ni kufika hatua ya makundi, jambo ambalo walishalitimiza na mkakati wa pili ni kushinda ubingwa wa ligi kuu na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, ambako amesema nafasi bado iko wazi kwao.

Simba imerejea nchini kutokea nchini Misri ambako ilipoteza mchezo wake dhidi ya Al Ahly kwa mabao 5-0, ambapo sasa itafanya maandalizi ya mchezo wa marudio dhidi waarabu hao utakaopigwa Februari 12 katika uwanja wa taifa. Baada ya mchezo huo itaanza kampeni ya kupunguza mechi zake za viporo vya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo ipo nyuma kwa michezo 7 dhidi ya mahasimu wao Yanga.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad