Kwa mujibu wa Kaimu Katibu wa Vijana Chadema mkoa wa Morogoro, Jackson Malisa, Wabunge hao walikamatwa Jumatano iliyopita ya Februari 20, 2019 wakiwa Kijiji cha Sofi wilaya ya Malinyi na kukaa rumande hadi leo Jumatatu Februari 25, 2019.
Bado haijafahamika wabunge hao na wenzao wana tuhuma gani, lakini wiki iliyopita Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alisema jeshi hilo lilikuwa linawasaka wabunge hao pamoja na wanachama 11 wa Chadema walioachiwa huru na mahakama mkoani humo Januari 2019.
Waliachiwa huru kupitia kifungu cha Sheria namba 225 cha mwenendo wa makosa ya jinai baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yanawakabili, ikiwa ni pamoja na kuchoma moto ofisi ya Sekondari ya kijiji cha Sofi Wilaya ya Malinyi.
Mutafungwa alisema kuwa jeshi la Polisi hivi sasa wamejipanga kwa kuwa na ushahidi na vielelezo vya kutosha vya kuwatia hatiani watuhumiwa hao waliokuwa wameachiwa huru na Mahakama.