Manchester United lazima wafanye kazi ya ziada kufufua ndoto yao ya kushinda taji ya kombe la Champions baada ya kufungwa mabao 2- 0 na Paris St-Germain katika uwanja wa Old Trafford.
Mabao ya Presnel Kimpembe na Kylian Mbappe yaliwapatia ushindi mabingwa wa Ufaransa.
Ushindi wa mara 10 wa United katika mechi 11 chini ya meneja wao wa muda Ole Gunnar Solskjaer ulifufua matumaini yao ya kuwa tena mabingwa wa ulaya.
Hata hivyo matumaini hayo yalizimwa na PSG katika uga wa nyumbani kwa zaidi ya bao moja.
Sasa United wanahitaji miujiza watakapokutana tena na miamba hao wa Ufaransa mjini Paris Machi 6 ili wafuzu kuingia robo fainali.
Matumaini ya Solskjaer yalididimizwa na majeruhi ya Jesse Lingard na Anthony Martial katika kipindi cha kwanza lakini PSG waliimarisha mashambulizi yao bila uwepo kwa wachezaji nyota wao Neymar na Edinson Cavani.
Kitumbua cha United kiliingia mchanga zaidi, baada ya Paul Pogba kutupwa nje dakika za mwisho za muda wa ziada kwa kulishwa kadi ya njano mara pili katika hatua ambayo itamkosesha mechi ya marudio.
Solskjaer amefanya kazi ya kuwatia motisha wachezaji baada ya Jose Mourinho kufutwa kazi mwezi Disemba - lakini usiku wa Jumanne ya Februari 12 ulikuwa mrefu kwake tangu alipotua Old Trafford.
United hawastahili kulaumiwa kwa kushindwa, kilichojitokeza katika mechi hiyo ni kwamba hawakuwa na ubavu wa kukabiliana na timu ya Thomas Tuchel hasa baada ya ya lango lau kushambuliwa na kupitia utendakazi wa Di Maria na kasi ya Mbappe.
Matumaini ya Solskjaer kufanya vyema katika mechi ya marudio huenda yangalipo lakini hali ilivyo kwa sasa huenda kipigo hiki kimetia kikomo azma ya Manchester United kushida taji la Champions.
Di Maria alihamia Manchester United baada ya kununuliwa wakati huo katika uhamisho wa kuvunja rekodi Ungereza wa £59.7m kutoka Real Madrid.
Lakini nyota huyo wa Argentina hakutumiwa vizuri na meneja wa wakati huo wa United Louis van Gaal, hali ambayo ilimfanya kuhamia PSG kwa mkataba wa £44.3m.
Angel di Maria akisherehekea ushindi wa PSG dhidi ya Manchester United uwanjani Old Trafford
Manchester United na mashabiki wao walishuhudia kile ambacho angeliwafanyia laiti angelikuwa mchezaji wao wakati wa mechi yao dhidi ya PSG.
Mashabiki wa klabu hiyo walimshangilia kwa kuonesha thamani yake katika mechi hiyo.