BARCELONA wanatarajiwa kuwakaribisha Real Madrid kwenye Dimba la Camp Nou leo kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali wa Copa del Rey.
Huu utakuwa mchezo wa pili wa Clasico kwa msimu huu wa 2018-19, huku Barcelona wakiwa na rekodi ya kupata ushindi mnono wa mabao 5-1 mwaka jana kwenye ligi. Barcelona watakuwa wakiingia kwenye mchezo huu wakiwa ndiyo mabingwa watetezi baada ya kuutwaa ubingwa huo kwa mara ya 30 msimu uliopita.
Hata Hivyo, Barcelona wanaonekana kuwa kwenye kasi nzuri sana kwa sasa kwenye La Liga tofauti na Madrid ambao wanasuasua. Hii itakuwa mara ya kwanza timu hiyo zinakutana kwenye kombe hilo tangu walipofi ka fainali mwaka 2013-14, ambapo Barcelona walipata ushindi wa mabao 2-1.
Wachezaji wa Barcelona, Rafi nha na Samuel Umtiti wataukosa mchezo huo, huku taarifa ya Barcelona ya jana usiku ikisema kuwa bado haijafahamika kama Lionel Messi anaweza kuwa uwanjani kwenye mechi hiyo.
Madrid wenyewe wanaonekana wachezaji wao wengi watarejea uwanjani, Dani Carvajal na Raphael Varane ambao hawakucheza mechi ya wikiendi dhidi ya Alaves wanarudi uwanjani leo.
Pia Marcelo na Toni Krosi ambao walikuwa na majeraha nao wamerejea uwanjani. Barcelona inaweza kupangwa hivi: Ter Stegen; Semedo, Pique, Lenglet, Alba; Arthur, Rakitic, Busquets; Coutinho, Suarez, Messi.
Real Madrid inaweza kupangwa hivi: Navas; Carvajal, Varane, Ramos, Marcelo; Casemiro, Kroos, Modric; Lucas, Benzema, Vinicius. Wamekutana mara: 239 Madrid wameshinda: 95 Barcelona wameshinda: 93 Sare: 50