Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Jumanne Muliro amefunguka juu ya kusambaa kwa uvumi wa kukutwa vichwa vya watoto kituo cha polisi na kusema taarifa hizo hazikuwa za kweli.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza Kamanda Muliro amesema ni watu wachache ambao waliamua kutangaza taarifa hiyo ambayo baadaye ilileta sintofahamu kwa baadhi ya wananchi wa Mwanza.
Muliro amesema, "kuna watu walianzisha taarifa kuwa kuna watoto walikuwa wamekufa na vichwa vyao kukutwa kituo cha polisi uvumi ule uilisababisha watu zaidi ya 500 kukusanyika kuja kituo cha polisi lakini hawakuelewa."
"Pamoja na huduma za kiusalama tunazotoa ilitulazimu tutumie mabomu ya machozi ili kuwatawanya kwa sababu waligoma kuondoka lakini pia tunamshikiria watu kadhaa kwa ajili ya mahojiano ya tukio hilo." ameongeza Muliro.
Mara kwa mara kumekuwa kukiripotiwa matukio ya mauaji ya watoto katika baadhi ya mikoa nchini ambapo tayari imeshatokea katika Mkoa wa Simiyu pamoja na Njombe ambapo kupitia vyombo vya ulinzi husika tayari baadhi ya watuhumiwa wameshafikishwa mahakamani.
Mapema hivi karibuni Kamanda Jumanne Muliro alipokea kijiti cha nafasi hiyo ya Kamanda Mkoa baada ya aliyekuwa Kamanda wa Mkoa huo Jonathan Shana kuhamishiwa makao makuu ya polisi