Mahakama ya Rufani leo inatarajia kusikiliza rufaa iliyokatwa na Serikali kupinga uamuzi mdogo wa Mahakama Kuu wa kuendelea na usikilizwaji wa rufaa ya kufutiwa dhamana kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko.
Mbowe na Matiko, walifutiwa dhamana Novemba 23, mwaka jana na Hakimu Mkazi Mkuu katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Willbard Mashauri (sasa Jaji) kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana.
Mashauri aliyekuwa akisikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili vigogo hao na wenzao saba, aliteuliwa na Rais John Magufuli, Januari 27, mwaka huu kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Hata hivyo, baada ya Mbowe na Matiko kufutiwa dhamana, kupitia kwa Wakili wao, Peter Kibatala walikata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.
Baada ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote, upande wa serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alidai wamekata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi uliyotolewa na Mahakama Kuu kisha kuiomba mahakama hiyo kuacha kuendelea kusikiliza rufaa hiyo kwa sababu haina mamlaka.
Jaji Rumanyika alisema mahakama yake imefungwa mikono, hivyo anasitisha usikilizwaji wa rufani hiyo hadi itakapotolewa
uamuzi katika Mahakama ya Rufani.
Mbali na Mbowe na Matiko, washitakiwa wengine katika kesi ya uchochezi ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk
Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.
Wengine ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu ambao wote walikuwepo mahakamani.
Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka
13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018 maeneo ya Dar es Salaam.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo katika barabara ya Kawawa, Mkwajuni, Kinondoni, siku wakihitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni na kusababisha vurugu zilizosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.
Rufaa ya Ya Freeman Mbowe na Ester Matiko Kusikilizwa Leo
0
February 18, 2019
Tags