Sakata la Korosho Laibuka Tena Bungeni
0
February 03, 2019
Sakata la ununuzi wa korosho limeendelea kuwasha moto bungeni baada ya Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali kusema yupo tayari kujiuzulu ubunge iwapo itathibitika kwamba wakulima hawalipwi Sh2,640 kwa kilo badala ya Sh3,300 iliyotangazwa na Rais John Magufuli.
Akichangia taarifa za kamati za Bunge za Bajeti na ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) jana, Bobali alisema kwa taarifa zilizotolewa na Serikali ni wazi kuwa kilo moja ya korosho imeuzwa kwa Sh4,180 na kuitaka kueleza kama itaendelea kuwalipa wakulima korosho daraja la kwanza kwa Sh3,500.
“Tunataka kauli kama mmeuza kwa Sh4,180 hii iliyozidi mtawarudishia wakulima? Jambo la pili, hivi sasa ninavyozungumza wakulima wanalipwa Sh2,640 kwa kilo ya korosho sio tena Sh3,300,” alisema.
Hoja ya mbunge huyo ilimfanya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya kusimama akitumia kanuni ya 64 A na kusema kuwa Bobali amelidanganya Bunge.
Kauli hiyo ilizua kelele kwa baadhi ya wabunge kupinga kwamba kanuni hiyo iliyotumiwa na Manyanya haipo kwenye Kanuni za Bunge hali iliyomfanya Spika amruhusu Bobali kuendelea na kuchangia hoja yake.
Akiendelea kuchangia, mbunge huyo alikazia kauli yake ya awali kuwa wakulima wanalipwa Sh2,640 kwa kilo moja ya korosho badala Sh3,300 kama ilivyoahidiwa na Rais Magufuli.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga alisema kumekuwa na taarifa za upotoshaji juu ya bei ambayo Serikali inanunulia korosho.
Alisema wapo watu wengi wanasema wamenunua kilo moja ya korosho kwa Sh3,300 lakini si kweli kwa sababu ukijumlisha gharama zingine, inakuwa zaidi ya Sh3,600 kwa kilo.
“Nataka niseme kuwa bei tuliyonunulia si kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, utaratibu uliokuwapo ulikuwa ukishanunua kwa bei ya Sh3,300 ndiyo unaanza kutoa gharama za magunia na vitu vingine,” alisema Hasunga.
Alisema ukijumulisha ushuru (Export levy) ambao ni Sh360, kilo moja ya korosho inakuwa imeuzwa kwa zaidi ya Sh4,160 kwa kilo. Alisema hadi sasa, Serikali imeuza tani 100,000 za korosho na wanaendelea kuuza na kwamba, wakishawalipa watu wote watafahamu wamepata faida kiasi gani.
Tags