LEO kuna mechi 15 kwenye michuano Europa na mwanetu Mbwana Samatta yuko mzigoni. Genk leo saa 5 usiku itacheza na Slavia Prague nyumbani. Hiyo ni siku moja baada ya Samatta kutokea kwenye kurasa za magazeti mengi ya Ubelgiji jana Jumatano akiwasisitizia mashabiki kwamba atakuwemo ndani ya Genk miaka 10 ijayo wala wasiwe na wasiwasi.
“Nina raha kuwa hapa Genk na nitakaa hapa miaka kumi ijayo, lakini hapa vilevile siyo mwisho wangu,” Samatta aliwaambia waandishi wa habari.
“Nilikuwa naota kucheza Ulaya na nimefanikiwa, sina haja ya kujipa presha
kubwa, nimeshatekeleza ndoto yangu, hakuna anayejua yajayo,” alisema Samatta ingawa kiuhalisia ni kama anawazuga mashabiki hao kwani huenda akapata dili muda wowote.
Samatta kwa sasa ana mabao 20 katika ligi ya Ubelgiji huku kwenye Europa hatua hii ya 32 bora akiwa na mabao matatu.
Katika mechi ya kwanza na Slavia, Genk wakiwa ugenini Czech walitoka suluhu, lakini mashabiki wao leo wanaamini lazima Samatta atupie. KRC Genk hawajapoteza mchezo wowote katika michezo tisa iliyopita ya Europa wakiwa nyumbani kwenye uwanja wao wa Crystal wameshinda michezo sita na wametoa sare tatu. Lakini mchezaji wa Slavia, Josef Husbaer amepiga mashuti mengi kuliko mchezaji yeyote katika michuano ya Europa bila kufunga bao akiwa amefanya hivyo mara 17.