Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amekutana na Wakulima na Wawekezaji wa zao la parachichi katika Wilaya ya Rungwe, Mkoani Mbeya. Mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki uliwakutanisha wataalam kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali na wadau wote wa zao la Parachichi.
Waziri Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda unaoendana na maendeleo ya Sekta ya Kilimo na katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Mkakati wa Pili wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo, Serikali imeweka msukumo mkubwa kwenye mazao yenye thamani kubwa ikiwepo zao la parachichi.
Amesema nafasi ya sekta ya kilimo ni kubwa katika kujenga uchumi wa nchi, kutokana na ukweli kwamba theluthi mbili ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea kilimo, hivyo kuinua kilimo cha parachichi kitasaidia kuongeza ajira na kipato kwa vijana.
‘Parachichi ni zao jipya lakini lina thamani kubwa sana, ulimwenguni linajulikana kama dhahabu ya kijani’ alisema Dkt. Mpango.
Amewataka wakulima wa zao hilo kuhakikisha Tanzania inakuwa kinara wa uuzaji wa parachichi nje ya nchi ili kukuza uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.
"Ili kuzalisha kwa wingi zao hili Wakulima wetu hasa wadogo wadogo wanatakiwa wawe na mitaji, utaalamu, sehemu ya kuhifadhia mazao yao na kuwepo na masoko ya kuuzia zao hilo, hasa masoko ya nje ambayo yataingizia nchi fedha za kigeni" aliongeza Dkt. Mpango
Mhe. Mpango amesema Serikali itaendeleza sekta ya kilimo kwa kuwa ndio sekta mama katika Taifa, inayozalisha malighafi za viwandani na kuliingizia fedha nyingi za kigeni.
Awali akimkaribisha Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila amesema Mkoa wa Mbeya ni ukanda maalum katika mazao ya Kilimo, ukiacha zao la Parachichi ambalo linazalishwa kwa wingi Wilayani Rungwe, pia Wilaya hiyo ni maarufu kwa kilimo cha ndizi na viazi, mazao ambayo yanatoa fursa kubwa kwa kutoa ajira kwa wananchi wa Mbeya na kukuza uchumi wa Taifa.
Kikao hicho cha wawekezaji na wakulima wa zao la Parachichi mkoani Mbeya, kimehudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Godfrey Mwambe.
Serikali Yapania Kuinua Zao La Parachichi Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya
0
February 19, 2019
Tags