Serikali Yasema Imejipanga Kukabili Maafa nchini

Serikali imedhamiria kuendelea kuchukua hatua za upunguzaji wa athari za maafa kwa kuwa ni moja ya eneo lililopewa kipaumbele katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka wa Mitano, 2016/17- 2020/21.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kanali Jimmy Matamwe alipokuwa akifunga warsha ya kupunguza madhara ya maafa nchini na kuimarisha uthabiti kwa nchi na jamii dhidi ya majanga ya asili katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara Februari 1, 2019 Jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa, hatua hiyo ni muhimu katika mkakati wa upunguzaji wa madhara yatokanayo na maafa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya msingi ya Mfumo wa Sendai wa Kupunguza Madhara ya Maafa wa mwaka 2015 – 2030 sambamba na malengo endelevu ya mwaka 2030 na makubaliano ya Paris juu ya mabadiliko ya tabianchi.

“imeelezwa kuwa mmepata fursa ya kuandaa mkakati  wa kupunguza madhara mafuriko na ukame kwa kutumia taarifa ya muhtasari wa vihatarishi mlioujadili na hii imetoa fursa ya kujiamini katika kusimamia na kutatua majanga haya ambayo yamekuwa yakiikumba nchi mara kwa mara na kusababisha hasara kubwa za kiuchumi na kuongeza wigo wa umasikini nchini”,alisema Kanali Matamwe

Katika kuhakikisha mipango hiyo inakuwa endelevu Kanali Matamwe alitoa rai kwa washiriki wa warsha hiyo kuainisha maeneo yanayohusu sekta zao na kuyafanyia kazi katika mipango ya bajeti na kuendelea kuongeza nguvu kwa kutenga bajeti ya kutosha katika masula ya kukabiliana na majanga.

“Tukumbuke uwekezaji katika kupunguza madhara ya maafa ni hatua muhimu katika kupunguza matumizi ya fedha nyingi kwa ajili ya kukabiliana na madhara ya yanayoweza kutokea”,alisisitiza Kanali Matamwe

Serikali kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na.7 ya mwaka 2015 na kanuni za usimamizi wa maafa za mwaka 2017 zimeanzisha Kamati za Usimamizi wa maafa ngazi ya Mkoa hadi Kijiji kwa lengo la kupunguza madhara ya maafa ili kuwa na jamii stahimilivu.

Kwa upande wake mshiriki wa warsha hiyo Bw. John Kiriwai alieleza kuwa, kuna umuhimu wa kuwekeza nguvu na fedha katika masuala ya maafa kulingana na takwimu na taarifa zinazoeleza umuhimu wa kuwa na mikakati madhubuti ili kuwa mipango endelevu katika kukabili maafa.

“Ni wakati sasa kuendelea kutumia fursa zilizopo kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa na kutumia taarifa za watafiti mbalimbali na kuziweka katika mipango yetu ya maendeleo ili kupunguza athari za maafa,”alisema Kiriwai.

Naye Mwakilishi kutoka Wakala wa Barabara Bi.Zaharani Madai alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hawana budi kuendelea kuwa na jitihada za makusudi za kuimarisha miundombinu kwa kuzingatia mazingira yaliyopo kwa kutumia wataalam katika kujenga na kuimarisha maeneo yanayodhaniwa kuwa hatarishi pindi maafa yanapotokea.

“Ni wakati sasa wa kujijenga upya ili kuwa na mikakati inayotekelezeka katika kutatua na kukabili maafa kwa kuimarisha miundombinu tuliyonayo ili kuendana na mazingira ya kukabili maafa nchini,”alisisitiza Madai.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad