Sheikh Ponda aulalamikia uongozi UDOM kwa Kusitisha Ujenzi wa Msikiti

Sheikh Ponda aulalamikia uongozi UDOM kwa Kusitisha Ujenzi wa Msikiti
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania imeeleza kusikitishwa na kitendo kilichofanywa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuamua kusitisha ujenzi wa msikiti uliokuwa ukijengwa katika chuo hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Jumuiya hiyo Sheikh Issa Ponda alisema, mwaka 2016 uongozi wa chuo hicho uliwapatia ekari 10 baada ya kukubali ombi la jumuiya hiyo la kutaka kujenga msikiti huo.

Ponda alisema, walianza kushughulikia vibali vya ujenzi katika mamlaka za chuo hicho na nje na walifanikiwa kuvipata vyote na mwaka jana waliwasilisha nyaraka za ujenzi kwa menejimenti ya chuo na kuingia mkataba na mkandarasi ambaye alianza kujenga kwa kuweka uzio wa mabati.

Katibu huyo alisema kuwa Januari 9, mwaka huu walishangazwa baada ya uongozi wa Udom kuwaita na kuwataka kusitisha ujenzi huo.

Alisema kuwa amri hiyo ilikuwa imetolewa na Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Gaudensia Kabaka kwa madai kuwa ombi hilo lilikubaliwa na uongozi uliopita na sio wa sasa.

Alisema baada ya kikao hicho, uongozi wa chuo hicho uliamua kuvunja uzio wa msikiti huo chini ya usimamizi wa polisi.

“Jumuiya tumeazimia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulaani tukio hilo, Pia tunaitaka Serikali iwabane waliohusika ili walipe gharama za ujenzi na kutoa tamko rasmi kuhusu hatua hiyo,” alisema.

Akizungumzia tuhuma hizo, Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Gaudensia Kabaka amesema  kilichofanyika na watu hao ni kukiuka taratibu na hawakupewa kibali na mamlaka husika kujenga nyumba hiyo ya ibada.

“Kile kiwanja kipo ndani ya chuo na wao hawakuwa na idhini wala kibali cha ujenzi. Pia hakukuwa na bango lolote linaloonyesha kuwa kuna ujenzi na mkandarasi ni nani, ndio maana walikuwa wanapitisha malighafi zao usiku na polisi hawakutumika kuvunja uzio bali walinzi wa Suma- JKT,” amesema.

Kabaka amefafanua kuwa eneo hilo, liliachwa wazi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kuabudu kwa dini zote mbili, lakini uongozi wa chuo ulikuwa bado haujatoa mwongozo wa ujenzi kwa kuwa walikuwa wakiendelea na vikao vya kujadili mchakato huo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad