Simba yaikamata Yanga kileleni ligi kuu
0
February 04, 2019
Kimahesabu inaonesha Yanga inaweza kukamatwa kileleni na Simba baada ya kushidwa kuondoka na pointi tatu hii leo dhidi ya Coastal Union.
Yanga imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga. Coastal Union wakiwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Haji Ugando katika dakika ya 30 ya mchezo huku bao la Yanga likifungwa na Matheo Anthony katika dakika ya 76.
Baada ya matokeo hayo, sasa Yanga inafikisha pointi 54 baada ya kucheza michezo 21, huku mahasimu wao Simba wakiwa na pointi 33 katika michezo 14 waliyocheza mpaka sasa. Simba ina viporo vya michezo 7 kufikia idadi ya michezo ya Yanga, endapo itafanikiwa kuibuka na ushindi katika michezo yote iliyobakia itafikisha pointi 54 sawa na Yanga iliyopo kileleni.
Nafasi ya pili inashikiliwa na Azam FC yenya pointi 47, nafasi ya tatu ni KMC yenye pointi 35 na Simba ikiwa katika nafasi ya nne kwa pointi 33.
Viporo vya Simba vimetokana na kuwa na ratiba ya michuano ya kimataifa ya Klabu Bingwa Afrika, ambapo hivi sasa ipo katika hatua ya makundi. Inatarajia kurejea hivi karibuni kutokea nchini Misri ilikokwenda kucheza mchezo wake wa Klabu Bingwa dhidi ya Al Ahly na kufungwa mabao 5-0.
Timu hizo zinatarajia kukutana katikati ya mwezi huu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo mchezo wa kwanza masimu huu ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Tags