KUELEKEA kwenye mchezo wa leo Jumamosi saa 4 Usiku kwa saa za Kitanzania kati ya Simba na wenyeji Al Ahly ya Misiri, wachezaji wameapa kupambana ili wasirudie makosa waliyofanya katika mchezo uliopita.
Simba katika mchezo uliopita walifungwa mabao 5-0 na AS Vital ,ukiwa ni mchezo wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, leo watacheza mechi ya tatu na Al Ahly kwenye Uwanja wa Borg El Arab.
Simba sasa wapo nafasi ya tatu kwenye kundi lao wakiwa na pointi tatu wakati Ahl Ahly ni vinara wakiwa na alama nne, AS Vita ya pili na pointi zao tatu huku JS Saoura wakiwa mkiani na alama yao moja.
Wakizungumza na Championi Jumamosi kwa nyakati tofauti mastaa wa Simba wakiongozwa na Mkude wameweka wazi kwamba, wapo Misri kwa lengo la kupambana na kupata ushindi ambao utawaweka kwenye nafasi nzuri ya kucheza robo fainali.
Naye beki ‘jumba’, Pascal Wawa raia wa Ivory Coast alisema akili yao yote ipo kwenye mchezo huo kutokana na maandalizi waliyoyafanya huku akisisitiza hawataki kitokee kilichotokea nchini DR Congo katika mchezo dhidi ya As Vita.
“Tumejipanga vyema na kila kitu kipo sawa kabisa kama ilivyo kawaida yetu kila mechi mpango wetu ni kushinda hivyo tutapambana mpaka hatua ya mwisho kupata matokeo bila kuwadharau wapinzani wetu tunajua wako vizuri lakini sisi pia tunahitaji kushinda,” alisema Mkude.
Naye Wawa alisema: “Tunacheza dhidi ya timu ngumu Afrika, lakini hilo haliwezi kuwa kikwazo kwetu kushindwa kupambana dhidi yao kwa sababu huku tumefuata matokeo mazuri kwa upande wetu maana tumejifunza kilichotokea Congo sasa hatutaki kuona kinajirudia hapa.”