TAKUKURU Yaomba Kumhoji Mshitakiwa Kesi ya kutakatisha fedha inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa zamani NIDA

TAKUKURU Yaomba Kumhoji Mshitakiwa Kesi ya kutakatisha fedha inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa zamani NIDA
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,imekubali mshtakiwa wa tano, Xavery Kayombo, katika kesi ya kutakatisha fedha inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake watano, kwenda kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Amri hiyo ilitolewa jana Februari 12,2019 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally, baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha maombi kwamba mshtakiwa huyo anakwenda kuchukuliwa maelezo yake.

Wakili wa Serikali, Leonard Swai, alidai kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kutajwa na upande wa Jamhuri unaomba kibali cha kumchukua mshtakiwa kwenda kumhoji Takukuru.

Hakimu alisema mahakama yake imekubali mshtakiwa huyo kwenda kuhojiwa kwa siku moja kisha apelekwe mahabusu.

Alisema kesi hiyo itatajwa Februari 19, mwaka huu na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Baada kesi hiyo kupigwa kalenda, ndugu na wanafamilia wa washtakiwa walilalamikia hatua ya mahakama kuendesha kesi hiyo katika chumba kidogo badala ya ukumbi wa mahakama ya wazi.

Baadhi yao waliangua vilio kutokana na kukosa kuonana na ndugu zao walioko mahabusu, huku wakidai kuwa wamesafiri kutoka mikoani kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.

“Tumetoka Mbeya kuja kusikiliza kinachoendelea katika kesi za ndugu zetu, lakini tumeshindwa kusikia kwa sababu ya watu kufurika katika chumba kidogo walipoingia washtakiwa,” alisema mmoja wa wanaodaiwa kuwa wanafamilia wa washtakiwa hao huku akiangua kilio.

Mbali na Maimu na Kayombo washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Biashara wa (NIDA), Aveln Momburi, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond.

Awali washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 26 likiwamo la uhujumu uchumi, ila Januari 28,2019 waliachiwa huru na mahakama hiyo baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kusema hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.

Hata hivyo, baada ya washtakiwa kuondolewa mashtaka hayo na kuachiwa huru walikamatwa tena na walifikishwa katika mahakama hiyo kisha kusomewa mashtaka mapya 100 yakiwamo 25 ya utakatishaji fedha.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad