Tamko la Waziri wa Afya Katika Maadhimisho ya Saratani Duniani

Tamko la Waziri wa Afya Katika Maadhimisho ya Saratani Duniani
Siku ya Saratani Duniani huadhimishwa kila Tarehe 4 mwezi Februari. Siku hii, ambayo ilianza kuadhimishwa mwaka 2000 mjini Paris, Ufaransa wakati wa mkutano wa Dunia wa Saratani, ni siku maalumu ya kutafakari na kuuelezea ulimwengu hasa wananchi kuhusu janga la Saratani.

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani kwa mwaka huu wa 2019 ni:Ni Mimi, nitafanya (I am, I will) Binafsi, nitafanya jitihada zote kupunguza janga la Saratani Duniani.

Ujumbe huu unaeleza kwamba, kila mtu binafsi ana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika kupambana na janga la saratani kwa kuelimisha jamii, kuwa na mtazamo chanya, kupima afya yake, kujikinga na vitu vyote vyenye kusababisha saratani, kusaidia wagonjwa wa saratani na kwa Hospitali zote zinazotoa huduma ya saratani kuhakikisha zinatoa huduma bora, ili kupunguza janga la saratani na athari zake zote.

Saratani ni ugonjwa ambao unaathiri watu wa rika na jinsia zote; watoto, watu wazima, wake kwa waume. Takwima mpya za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (International Agency for Research on Cancer – IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO) zilizotolewa Septemba 2018, zinaeleza kwamba kila mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wa saratani wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1, na kati ya hao, zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki kutokana na ugonjwa wa saratani kila mwaka.

Aidha, watu zaidi ya millioni 43.8 wanaishi na saratani duniani kote na kama hatua madhubuti za kinga, uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la saratani litaongezeka na kufikia makadirio ya wagonjwa wapya milioni 24 ifikapo mwaka 2035, huku ongezeko kubwa likiwa katika ukanda wa nchi zinazoendelea kama Tanzania.

Nchini Tanzania, tatizo la saratani limekuwa likiongezeka na kukua siku hadi siku. Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC), zinaonyesha kwamba kwa Tanzania kunatokea mgonjwa 1 wa Saratani kwa kila watu 1000; hivyo Tanzania inakua na wagonjwa wapya wa Saratani 55,000 kwa mwaka na takribani wagonjwa 28,610 hufariki kwa mwaka, ambapo ni vifo asilimia 52 ya wagonjwa wapya.

Takwimu za hospitali za mwaka 2018, zinaonyesha wagonjwa wapya wa saratani waliohudumiwa ni 14,028 ambayo ni sawa na asilimia 25.5 ya wagonjwa wote wanaokadiriwa kuwepo nchini.

Wagonjwa waliohudumiwa walifika kupata huduma katika hospitali za Ocean Road (7,649), Bugando (2,790), KCMC (1,050), Muhimbili (1,321), na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (218). Aidha takribani wagonjwa wapya 1,000 walipata huduma katika hospitali binafsi za Agakhan, Hindu Mandal, Hubert Kairuki, Besta, Rabininsia na mikoani.

Aidha, Wagonjwa wengi takribani asilimia 75 walifika katika Hospitali wakiwa katika hatua za juu za ugonjwa (hatua ya 3 na ya 4) hali ambayo hupunguza uwezekano wa wagonjwa kupona maradhi yao. Hili ni tatizo kubwa ambalo tunaweza kuondokana nalo endapo tutakuwa na tabia ya kupima afya zetu mara kwa mara ili ugonjwa uweze kugundulika katika hatua za mwanzo na hivyo kutibika kwa urahisi.

Taarifa kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonesha kwamba kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa Saratani mwaka hadi mwaka. Mfano Mwaka 2015 wagonjwa wapya 5,764; mwaka 2016 wagonjwa wapya 6,338; mwaka 2017 wagonjwa wapya 7,091; na mwaka 2018 wagonjwa wapya 7,649.

Aidha kwa mujibu wa Taarifa kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road za mwaka 2018, aina za Saratani zinaoongoza hapa nchini ni kama ifuatavyo:

1. Saratani ya mlango wa kizazi (Cervical cancer) – 31.2%
2. Saratani ya matiti (Breast cancer) – 12.9%
3. Saratani ya koo (Cancer of the oesophagus) – 9.8%
4. Saratani ya ngozi (Kaposis Sarcoma) – 9.3%
5. Saratani za kichwa na shingo (Head and Neck) – 6.8%
6. Saratani ya matezi (Lymphoma) – 5.3%
7. Saratani ya damu (Leukemia) – 4.7%
8. Saratani ya tezi dume (Prostate cancer) – 3.9%
9. Saratani ya kibofu (Urinary Bladder cancer) – 2.8%
10. Saratani ya ngozi (Skin Cancer) – 2.6%

Mwaka 2018, Saratani ya Koo (Cancer of the Oesophagus) imejitokeza sana na kuwa Saratani ya 3 (9.8%) kati ya Saratani kubwa 5 kwa kuathiri watanzania wengi; kwa miaka ya nyuma ilikua saratani ya 4.

Kwa upande wa Wanaume, Saratani zinazoongoza ni:
Saratani ya Ngozi (Kaposi Sarcoma) (20.3%)
Saratani ya Koo (Esophageal Cancer) (18.7%)
Saratani ya Tezi Dume (Prostate Cancer) (16%)
Saratani ya matezi (Lymphoma) (13%)

Kwa upande wa wanawake, wengi wanaumwa Saratani:
1. Saratani ya Mlango ya Kizazi (Cervical Cancer) (56.5%)
Saratani ya Ngozi (Kaposis Sarcoma) (14%)
Saratani ya Matiti (Breast Cancer) (17%)
Saratani ya Koo (Esophageal Cancer) (11%)

Vyanzo vikubwa vya saratani vipo vinne;
Maambukizi (infection) – Maambukizi yamegawanyika katika sehemu kuu tatu;
Virusi – Kirusi ya Human Papilloma (Human Papiloma Virus) vinavyosababisha Saratani ya Mlango wa kizazi, na Kirusi cha Hepatitis B (Hepatitis B Virus) huweza kusababisha Saratani ya Ini.
Maambukizi ya Bakteria – Mfano Helicobacter Pyroli vinaweza kusababisha Saratani ya Tumbo.
Parasaiti (Parasites) – Kwa mfano vimelea vya kichocho vinaweza kusababisha Saratani ya Kibofu cha mkojo.

Kutokuzingatia Mtindo bora wa maisha (unhealthy Life Style), kama vile matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, kula vyakula ambavyo si salama au kula vyakula ambavyo havikuhifadhiwa vizuri, kutokula matunda na mbogamboga, kunywa pombe kupitiliza, matumizi ya dawa za kulevya na kutokufanya mazoezi.

Mfano, matumizi ya Tumbaku ni kisababishi kikubwa cha magonjwa ya Saratani ya matiti, mdomo, koo pamoja na magonjwa ya moyo. Unywaji wa vilevi uliopitiza huchangia kwenye kusababisha magonjwa ya saratani za matiti, ini, utumbo mpana, pamoja na saratani nyingine.

Madhara kutokana na Mazingira (Exposures) – Mfano miale ya jua ambayo inaathiri ngozi haswa kwa watu wanaoishi na ualbino huweza kusababisha saratani ya ngozi kwa jamii hii; vumbi la asbestos kutoka viwandani kusababisha saratani ya mapafu; kemikali za benzene katika mafuta ya mitambo kusababisha saratani ya damu; sumu kuvu kutoka katika nafaka kusababisha Saratani ya koo; n.k.

Urithi katika familia (vinasaba-Genetics) – Kwa mfano Saratani ya Matiti, Utumbo mpana, na tezi dume huweza kusababishwa na vinasaba kwenye ukoo mtu anaotokea.

Serikali inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, ambayo inapitiwa upya pamoja na mengineyo lengo likiwa ni kuhakikisha afua mbalimbali za afya zinajielekeza katika kutoa huduma bora zaidi na za kisasa kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo Saratani.

Aidha, Serikali, inaendelea kushirikiana na Mashirika ya Kimataifa, Mashirika yasiyo ya kiserikali na Sekta binafsi, kuandaa na kurekebisha Sheria, Kanuni na taratibu ili kuimarisha uzuiaji na udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Kwa upande wa kinga dhidi ya saratani, Serikali imeanza kutoa chanjo ya kukinga wasichana na virusi vinavyosababisha saratani ya mlango wa kizazi (HPV Vaccine) kuanzia mwezi Aprili 2018.

 Chanjo hii inatolewa kwa wasichana walio shuleni na kwenye jamii kuanzia umri wa miaka 9 hadi miaka 14. Hata hivyo kutokana na changamoto ya upatikanaji wa dozi za kutosha za chanjo hii kutoka kwa wazalishaji, Serikali iliamua kuanza kutoa chanjo hii kwa wasichana wa umri wa miaka 14 ambapo tulilenga kuwafikia wasichana wapatao 625,452 kwa mwaka 2018.

Kwa takwimu za awali, mpaka kufikia Desemba, 2018 wasichana wapatao 412,016 (66%) walipatiwa dozi ya kwanza na wasichana 125,362 (53%) ndiyo walikuwa wamekwishapatiwa dozi ya pili ya chanjo hii. Kutokana na chanjo kuanza kutumika mwezi Aprili 2018, lengo la mwaka litakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi, 2019.

Ninapenda kuwahimiza wazazi, walezi na walimu kuhakikisha wasichana wanaostahili kupata chanjo hii wanaipata bila vikwazo vyovyote. Hatua hii ya kuwapatia wasichana chanjo ya HPV itasaidia sana kupunguza au kutokomeza kabisa Saratani ya mlango wa kizazi hapa nchini kwetu.

Kwa upande wa kugundua mapema na kutibu mapema (Early detection and Early treatment), Serikali imeanzisha huduma kwenye vituo 624 vilivyopo katika Halmashauri mbalimbali nchini ambapo jumla ya wanawake 375,522 walifanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti mnamo mwaka 2017, ukilinganisha na wanawake 416,841 waliofanyiwa uchunguzi huo mwaka 2018. Kati ya hao, wanawake 16,147 waligundulika kuwa na mabadiliko ya awali mwaka 2017, na wanawake 18,341 mwaka 2018.

 Aidha wanawake 3,254 walidhaniwa kuwa na saratani ya mlango wa kizazi (suspicious cervical cancer) mwaka 2017, kulinganisha na wanawake 4,487 mwaka 2018 na hivyo kupatiwa rufaa Hospitali za ngazi za juu kwa ajili ya kuthibitisha kama ni saratani ili wapatiwe matibabu stahiki.

Hata hivyo licha ya kupewa rufaa, wanawake wengi bado hawaendi Hospitali kwa ajili ya ugunduzi na matibabu. Nitoe rai kwa wanawake kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zao ikiwemo Saratani ya Mlango wa Kizazi na Saratani ya Matiti angalau mara moja kwa mwaka, na wakigundulika na mabadiliko ya awali ya saratani, basi wasiache kwenda kupatiwa matibabu. Saratani ya mlango wa kizazi ikigundulika mapema, inatibika kwa asilimia 100.

Hivyo ninarudia tena kuwataka Waganga Wakuu wa Mikoa/Wilaya na Waganga Wafawidhi kuhakikisha Vituo vyote vya Afya (Health Centres) na Hospitali za umma nchini zinakuwa na siku maalum kila mwezi kwa ajili ya upimaji wa Saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti. Ugunduzi wa mapema wa saratani huokoa maisha.

Kwa upande wa matibabu, Serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt John Pombe Magufuli, kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwa kushirikiana na wadau wengine wa Maendeleo imehakikisha upatikanaji wa matibabu ya Saratani kwa wagonjwa wote kwa ufanisi zaidi. Mwaka 2018, Wizara ilinunua mashine mbili za kisasa za tiba ya Saratani aina ya LINAC zenye thamani ya shilingi bilioni 9.4 na kuzifunga katika Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Mashine hizi zilianza kufanya kazi mwezi Septemba 2018. Hadi kufikia Desemba 2018, jumla ya wagonjwa 109 wametibiwa kwa kutumia mashine hizi na kati ya wagonjwa hawa, wagonjwa 70 wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu endapo mashine hizi zisingekuwepo nchini kwa gharama za wastani wa Shilingi Milioni 50 kila mgonjwa.

Utumiaji wa mashine mpya za LINAC umeokoa Shilingi Bilioni 3.5 katika kipindi cha Septemba hadi Desemba 2018 tu. Pamoja na kuokoa fedha, pia muda wa kusubiri kuanza tiba za mionzi kwa wagonjwa umepungua hadi kuwa chini ya wiki 4; na tunategemea utakuwa chini ya wiki 2 ifikapo Aprili 2019. Mwaka 2015, muda wa kusubiri tiba mionzi ulikuwa wiki 12 na sasa tumeweza kuupunguza hadi kufikia wiki 4.

Serikali katika Mwaka wa fedha wa 2018/2019 imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa dawa za tiba ya Saratani kwa kuweka bajeti ya Shilingi bilioni 10, kutoka shilingi milioni 700 mwaka 2015/16 Kutokana na ongezeko hili la fedha, kiwango cha upatikanaji wa dawa za Saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road ni asilimia 92 kutoka asilimia 4 mwaka 2015. Aidha, mgao wa dawa za Saratani unapelekwa pia katika Hospitali za Bugando na KCMC.

Aidha, Serikali iko kwenye taratibu za kununua mashine ya kisasa ya upimaji wa Saratani aina ya PET Scan kwa thamani ya shilingi bilioni 14 ambayo itafungwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road. Upatikanaji wa kipimo hiki nchini utapunguza gharama zitokanazo na kupeleka wagonjwa nje ya nchi hasa India kwani takriban asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani walikuwa wanapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kipimo hiki.

Hivyo, Serikali itaokoa takriban Shilingi bilioni 5 kwa mwaka zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya kulipia wagonjwa kwenda nje kwa kipimo hiki.

Wastani ya watanzania 500 huenda nje ya nchi kila mwaka kwa ajili ya kipimo cha PET/CT Scan ambapo gharama kwa mgonjwa mmoja inafikia mpaka shilingi 10,000,000 ikijumlisha gharama za safari, malazi, huduma hospitali na kipimo.

Katika jitihada zetu za kuhakikisha upatikanaji wa matibabu ya saratani kwa wananchi wengi zaidi, Serikali imeongeza wigo wa upatikanaji wa matibabu ya Saratani kutoka Hospitali ya Saratani Ocean Road na sasa huduma za matibabu ya Saratani zinapatikana Hospitali ya Kanda Bugando ambayo imefunga mashine ya tiba mionzi ambapo wagonjwa wa Kanda ya Ziwa wanapata huduma za tiba ya mionzi (radiotherapy) Hospitalini hapo sambamba na huduma za matibabu kwa njia ya dawa (Chemotherapy).

Aidha, Hospitali ya Kanda ya KCMC, Kilimanjaro na Hospitali ya Kanda Mbeya zinatoa huduma ya tiba ya Saratani kwa dawa (Chemotherapy); ambapo hatua inayofuata ni kujenga jengo maalum kwa ajili ya kusimika mashine za mionzi katika Hospitali ya KCMC.

Ili kuwa na mipango bora ya upatikanaji wa fedha za kutoa huduma za saratani hapa nchini, takwimu sahihi zinahitajika. Kuanzia mwezi Juni, mwaka 2018, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kuchukua taarifa za saratani katika hospitali za Ocean Road, KCMC, Bugando, Mbeya na Benjamin Mkapa kwa mfumo uitwao Population-based cancer registry. Mfumo huo utawezesha kutupatia taarifa ya aina na ukubwa wa saratani ya aina fulani, inawapata zaidi jinsia gani, na ipo katika Kanda au Mkoa gani.

Aidha, mfumo huu utatupa takwimu za uhakika zaidi kuhusu idadi ya watu wanaofariki kila mwaka. Hii itasaidia Serikali katika mipango ya kupambana na saratani.

Saratani haibagui jinsi wala hali ya mtu. Ni vyema kila mmojawetu akapima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya kiafya.

Endapo mtu atatambuliwa kuwa ana ugonjwa wa Saratani ninamuhimiza kutumia huduma za afya kulingana na ushauri atakaopewa na wataalam wa afya. Kwa wale ambao wameshajitambua kuwa na matatizo ya Saratani lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na ugonjwa wa Saratani.

Tunao Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Saratani (National Cancer Control Strategy wa mwaka 2013-2022, Mkakati wa kisera wa Tiba shufaa wa mwaka 2013 (Palliative Care Policy Guidelines) na Mwongozo wa Kitaifa wa Tiba ya Saratani wa mwaka 2018 (National Cancer Treatment Guidelines) ambao umekamilika na utazinduliwa hivi karibuni.

 Mikakati hii na Mwongozo ni Dira katika kuimarisha huduma za Saratani katika kukinga, kugundua mapema, kutibu, kutoa tiba shufaa na hasa kupanga manunuzi ya Dawa za Saratani kwa kuzingatia hali halisi ya Nchi yetu.

Katika maadhimisho haya ya Siku ya Saratani Duniani, napenda kuchukua fursa hii kuhimiza Watanzania wote kwenda kwenye vituo vya afya kufanya uchunguzi wa Saratani hasa Saratani ya mlango wa Kizazi, Saratani ya Matiti, Tezi dume na saratani nyingine mapema. Kuchelewa kufika Hospitalini huchangia ongezeko la vifo vya saratani. Kwa upande wetu Serikali tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kuwa huduma za Afya ya saratani zinaboreshwa na zinapatikana karibu zaidi na wananchi.

Mwaka huu 2019 tutazindua Mwongozo wa Kitaifa wa Tiba ya magonjwa ya Saratani (National Cancer Treatment Guidelines) ambao ndio utatumika nchi nzima kuanzia Zahanati, ikihusisha zaidi huduma za Kinga, hadi kwenye ngazi ya Hospitali za Mikoa na Kanda ambapo huduma za uchunguzi na tiba za saratani zinapatikana na kufikia Hospitali za Kitaifa ambapo huduma za kibingwa za saratani zinapatikana.

Nachukua fursa hii pia kuwashukuru wadau wote wanaoshirikiana na Serikali katika jitihada za kudhibiti ugonjwa wa Saratani hapa nchini. Ni matarajio yetu kuwa wataendelea kushirikiana nasi katika kudhibiti tatizo la saratani nchini.

Ni Mimi, nitafanya (I am, I will) Binafsi, nitafanya jitihada zote kupunguza janga la Saratani Duniani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad