Serikali nchini Bangladesh imezima zaidi ya tovuti 20,000 ambazo zimekuwa zikirusha maudhui ya ngono na michezo ya kamari, hatua hiyo ikitangazwa kama sehemu ya operesheni ya kumaliza biashara ya ngono.
Wiki iliyopita watoaji wa huduma za intaneti, waliondoa tovuti zote ambazo zinaonesha ngono, hii ni baada ya kuamrishwa na mamlaka ya kudhibiti mitandao ya mawasiliano nchini humo.
Waziri wa Mawasiliano nchini humo, Mustapha Jabbar amesema “Serikali tunataka kuwe na intaneti salama na safi kwa raia wote wa Bangladesh, ikiwemo watoto. Hii ni vita dhidi ya mitandao ya ngono na vitakuwa vita visivyoisha,”.
Mbali na tovuti hizo za ngono, pia mtandao wa kijamii maarufu nchini humo wa TikTok nao umefungwa huku mitandao ya Facebook, Instagram na YouTube ikichunguzwa.
“Tovuti chache zimezimwa kwa kuwa na mambo yasiyokubalika kimaadili. Tumeshauri watu wengine kutochapisha kitu chochote ambacho kinakiuka maadili yetu ya kijamii,”amesema Jabbar na kuongeza
“Tunachunguza kurasa za Facebook za humu nchini, mitandao ya Youtube na Instagram kama zinapotosha maadili hatutosita kuwafungia”.
Operesheni hiyo ilianzishwa mwaka jana, baada ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo kuamrisha tovuti za ngono kupigwa marufuku na kuzimwa.