Ufafanuzi Ndoa ya Prof Kapuya na Benyy Kinyaiya

MEKUWA na upotoshaji, ama wa makusudi, bahati mbaya au kwa kutojua, kusema kuwa mzee wetu, Profesa Juma Kapuya amepata jiko.

Prof Kapuya amewahi kushika nyadhifa kibao serikalini. Amekuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri akihudumia wizara mbalimbali; Elimu, Ulinzi, Habari, Michezo, Utamaduni na nyingine. Halafu ni profesa na alifundisha UDSM takriban miongo minne iliyopita.

Kweli muda huo wote Kapuya awe hajawahi kumiliki jiko? Eti leo ndiyo mseme kwamba amepata jiko! Hii kauli kiukweli si yenye kumtendea haki mzee wetu, kiongozi wetu na msomi wetu.

Usahihi ni kuwa mzee Kapuya ameongeza jiko. Na si vibaya kuongeza jiko ili mahanjumati yawe inaiva vema kwa wakati. Halafu mzee wetu hakutaka fujo, maana ameongeza jiko dogodogo. Watu walitaka aongeze mjiko mkuuuubwa! Mwenyewe kajiamulia kuchukua kajiko kadogo ambako kanamtosha matumizi yake kwa sasa.

Kwa nini ukimbilie jiko kuuubwa wakati unahitaji kajiko kadogo tu? Mzee Kapuya hajataka 'kuintatein' matumizi mabaya ya rasilimali majiko.

KUHUSU KINYAIYA

Kupanga ni kuchagua. Papaa Benny Kinyaiya ameona jiko linalomfaa ni kubwa. Benny yeye ndiye kapata jiko, halafu kaona atafute jiko size kubwa ili baadaye asipate shida ya kuongeza lingine.

Si mnaona mnavyosogoa kuhusu mzee Kapuya kuongeza kajiko kadogo? Benny hataki hayo, kwa hiyo amechagua jiko la kutosha limfae wakati wote.

Ila wana mnakata stimu; aliyejiongezea kajiko kadogo mwamsema na aliyejichagulia jiko kubwa mwamsengenya.

Mwathubutu kutamka kuwa eti jiko linalomfaa Benny limetwaliwa na Kapuya, kisha linalomstahili Kapuya limejibebea Benny. Hivi ninyi ndiyo mnaenda kuyatumia hayo majiko? Mwajifanya mwajua matumizi ya majiko kuliko wenye majiko yao.

Kongole mzee Kapuya kwa kuongeza jiko dogo linalokutosha. Pongezi nyingi kwa Benny kwa kupata jiko kubwa linalokutosha. Hayo ndiyo matumizi mazuri ya rasilimali majiko.

Ndimi Luqman MALOTO

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad