Upasuaji Mkubwa wa Ubongo Wafanyika MOI


Upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe kwenye Ubongo, kuziba Mishipa ya damu iliyopasuka kwenye Ubongo pamoja na upasuaji wa mgongo umefanywa na Madakatari bingwa kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking, nchini China.

Upasuaji huo umefanyika Jijini Dar es Salaam umechukua takribani saa tano, umefanyika kufuatia  ujio wa jopo la Madaktari bingwa watatu wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Peking cha China ambao waliwasili MOI wiki iliyopita, kwa lengo la kutoa mafunzo na kufanya Kambi ya siku moja ya upasuaji.

Dk. Nicephorus Rutabansibwa alizungumza katika chumba cha upasuaji MOI amesema ushirikiano kati ya MOI na Peking utakuwa wenye manufaa makubwa kwa sababu huduma zinazotolewa zitaendelea kuwa bora na Watanzania wataendelea kupata huduma hizo nchini bila ya kwenda nje ya nchi.

“Huu ni mwendelezo wa ushirikiano tulioingia na wenzetu hawa wa Peking mwaka jana, tunaamini tutabadilishana uzoefu na wenzetu hawa ambao wamepiga hatua kubwa kwenye teknolojia ya matibabu, kupitia ushirikiano huu, mbinu tunazopata zitatusaidia kuendelea kutoa tiba bora na kwa wakati kwa wagonjwa wetu,” alisema Dk. Rutabansibwa.

Dk. Rutabansibwa alisema jana waliwafanyia upasuaji wagonjwa watatu, akiwamo mmoja aliyefanyiwa wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kwa kutumia darubini ya kisasa, mwingine upasuaji wa mgongo na mwingine atafanyiwa upasuaji wa kuziba mishipa ya damu iliyopasuka kwenye kichwa.

Kambi hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa mkataba wa ushirikiano uliosainiwa kati ya MOI, Chuo Kikuu cha MUHAS na Hospitali ya Peking ya China ambao umejikita katika mafunzo ya muda mrefu na mfupi, utafiti, tiba pamoja na uboreshaji wa miundombinu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad