Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo Wawi Chake Chake Pemba, wakati wa majumuisho ya ziara yake kisiwani humo.
Alisema kuwa Uwanja huo utakuwa wa kisasa na mkubwa utakaoruhusu ndege za aina zote kubwa kutua katika kiwanja hicho na kusaidia usafiri wa anga.
Alisema tayari mchakato wake umeanza na ameshatuma mawaziri 10 kwenda kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa Uwanja huo wakiwamo wananchi wa Mfikiwa, Furaha na Mvumoni ili wakae tayari ujenzi utakapoanza waweze kuondoka katika eneo hilo na kupewa fedha kwa ajili ya mali zao.
Dk. Shein alisema kuwa tayari upembuzi yakinifu umeshafanywa kwa ajili ya uwanja huo mpya wa ndege na karibu Sh. milioni 500 zimetumika na hivi sasa serikali iko katika hatua za kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.
“Niwaombe wananchi kuwa na subira hasa wale wanaoishi pembezoni mwa uwanja huo kwa kuwa mtapewa fidia mara tu ujenzi utakapoanza,” alisema.
Aidha, Dk. Shein aliwataka wawakilishi wa majimbo yaliyoko katika Wilaya ya Chake Chake, Pemba kuongeza kasi ya kushirikiana kwa kwenda kufanya kazi ili kuwashughulikia wananchi kwa azma ya kutatua changamoto walizonazo.