Viongozi wa Jumuia ya Afrika ya Mashariki wanakutana baadaye leo mjini Arusha kaskazini mwa Tanzania, huku kukiwa na hali ya wasiwasi na uadui miongoni mwa nchi wanachama.
Katika siku za hivi karibuni Burundi iliitangaza Rwanda kama adui yake. Na kwa upande mwingine Rwanda imekuwa ikilalamikia juu ya kile inachosema vitendo vya utesaji, utekwaji na kurudishwa nyumbani kiholela kwa raia wake wanaosafiri nchini Uganda.
Wanachama wengine wa jumuia hiyo ya EAC ni pamoja na wenyeji wa mkutano Tanzania, Kenya na Sudan ya Kusini.
Sio viongozi wote wa mataifa sita wanachama watahudhuria mkutano huo wa leo. Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza atawakilishwa na naibu wake, wakati Rais wa Sudan kusini Salva Kiir naye atawakilishwa na ujumbe maalum.
Mkutano huu ulipangwa kufanyika Novemba mwaka jana lakini ukaahirishwa mara mbiili baada yab Burundi kuugomea. Burundi inalalamika kwamba jumuia inafumbia macho uhusiano wake mbaya na Rwanda, ambayo kwa sasa ndio nchi adui yake mkubwa katika eneo hili.
Haki miliki ya pichaAFP
Image caption
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi anamlaumu mwenziye wa Rwanda Paul Kagame kwa kufadhili jaribio la kutaka kumpindua madarakani miaka mitatu iliyopita pamoja na kutoa mafunzo kwa vikundi vya waasi vinavyovuruga usalama wa nchi hiyo.
Rwanda nayo haiko sawa na jirani zake Uganda. Mamlaka mjini Kigali zimekuwa zikilalamikia matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu dhidi ya raia wake wanaoenda Uganda.
Rwanda imekuwa ikikanusha madai ya Burundi, wakati Uganda haisemi lolote.
Nkurunziza asema Rwanda imekuwa adui
Mkutano wa kwanza unaojumuisha vijana wa jumuiya ya Afrika mashariki
Ratiba ya mkutano wa leo inaonesha kuwa kutazungumziwa masuala kuhusu kuanzishwa kwa sarafu ya pamoja na masuala mengine ya kisiasa ndani ya jumuia.