Viwanda 3,504 Vimeanzishwa Nchini


Jumla ya viwanda 3,504 vimeanzishwa nchini kutokana na juhudi za kujenga uchumi wa viwanda zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano tangu iingie madarakani hadi kufikia Desemba, 2018.

Hayo yameelezwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya alipokuwa  akijibu swali la mbunge wa Chumbageni, Mhe. Ussi Salum Pondeza juu ya viwanda vingapi vimeanzishwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano ianze utekelezaji wa mpango wa kuimarisha uchumi wa kati wa viwanda.

“Kati ya viwanda hivyo 3,504 vilivyoanzishwa, vinajumuisha viwanda vidogo sana 2,500, viwanda vidogo 943, viwanda vya kati 51 na viwanda vikubwa 10,” amesema Mhandisi Manyanya.

Amesema wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikifanya tathmini ya viwanda 156 vilivyobinafsishwa na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa kwa viwanda  68  ambavyo havijaendelezwa.

Aidha amesema, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilijiridhisha na mapendekezo yaliyotolewa na kuiwezeshsa Ofisi ya Msajili wa Hazina kuchukuwa hatua.

Mhandisi Manyanya  amesema hatua iliyochukuliwa na Ofisi ya Msajili ni kuvirejesha viwanda 14 Serikalini na juhudi za kuvitafutia wawekezaji wengine walio tayari kuviendeleza zinaendelea.

Ameeleza kuwa, kwa mujibu wa hali ya uchumi ya mwaka 2017, mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa ni asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 0.6.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad