SERIKALI ya Mkoa wa Iringa imetangaza kuwasaka wafanyabiashara wa mitandaoni kama moja ya mkakati wake wa siku 90 hadi Mei 7, mwaka huu, unaolenga kila anayefanya biashara mkoani humo alipe kodi au awe na kitambulisho cha machinga.
Mkakati huo ulitangazwa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi baada ya kupokea taarifa ya ugawaji wa vitambulisho 25,000 vya awali vya machinga katika hafla iliyohusisha ugawaji wa nyongeza ya vitambulisho vingine 35,000 kwa halmashauri tano za mkoa huo.
Taarifa hiyo inaonesha tangu vitambulisho hivyo vya awali 25,000 vianze kugaiwa kwa Sh 20,000 kwa wafanyabiashara ndogo wa halmashauri hizo Desemba mwaka jana, vitambulisho zaidi ya 9,000 vilikuwa vimeshachukuliwa hadi wiki iliyopita.
Akitangaza mkakati huo ambao lengo lake pia ni kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali, Hapi alisema; “Ndani ya mkoa wa Iringa hatutaki kuwa na mjasiriamali ambaye hayupo katika moja kati ya mifumo mitatu inayoiwezesha serikali kuwatambua.”
Alitaja mifumo hiyo kuwa ni ule wa leseni za biashara zinazotambuliwa na halmashauri, unaopitia Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo vilivyoanza kutolewa hivi karibuni na Rais John Magufuli.
Alisema anayefanya biashara bila kuwa na moja kati ya vitu hivyo vitatu, huyo hana tofauti na mhujumu uchumi na ni lazima atafutwe ili afuate utaratibu.
“Wanauza nguo, keki, vyakula, bidhaa za tiba za jadi na biashara yoyote ile mkoani kwetu kupitia mitandao ya kijamii, katika simu za mikononi na vifaa vingine vinavyotumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano, watatafutwa ili wasajiliwe katika moja ya mifumo hiyo,” alisema.
Alisema mzigo wa kuendesha nchi hii ni wa kila Mtanzania mwenye shughuli halali inayomuingizia kipato na akataja watu wengine ambao hawapaswi kusahaulika katika utaratibu huo kuwa ni wale wanaoendesha vikundi vya kuweka na kukopa fedha.
“Wanaokopa kwenye Vicoba kwa ajili ya shughuli za ujasiriamali lazima watafutwe na wapewe vitambulisho na kama biashara zao zina sifa za juu ya vitambulisho waingizwe kwenye utaratibu wa kulipa kodi kupitia TRA,” alisema.
Alisema mkoa umetoa muda wa miezi mitatu kwa wajasiriamali wote kuingia katika moja ya mifumo hiyo na “baada ya hapo tutafanya oparesheni kubwa ya kuwasaka wasio kwenye mfumo wowote kati ya hiyo.”
Aidha Mkuu wa Mkoa aliiagiza TRA kutumia pia siku hizo 90 kufanya msako wa wafanyabiashara walio katika mfumo wa Malipo ya Kielektroniki (EFDs); wanaouza bidhaa na huduma bila kutoa risiti za mashine