Waimbaji wa Muziki wa Injili Bongo Ambao Kwa Sasa Wanatikisa Kutokana na Nyimbo zao
0
February 14, 2019
KATIKA kila jambo au kazi kuna kuzidiana na kila mtu duniani ana wakati wake wa kuwa juu na kuonekana anafanya vizuri na kuna wakati wa kuonekana wa kawaida na mwisho unakuwa chini kabisa. Vivyo hivyo hata katika ulimwengu wa sanaa mbalimbali, hali hiyo ipo ambapo leo katika makala haya tunaangalia waimbaji wa muziki wa Injili Bongo ambao kwa sasa wanatikisa kutokana na nyimbo zao na kujikuta wakiwafunika wale waliozoeleka kama Rose Muhando, Bahati Bukuku, Upendo Nkone, Mchungaji Abiud Misholi, Epharaim Mwansansu, Bonny Mwaitege na wengine wengi. Hawa hapa chini ni wale wanaotikisa ambao ukikatiza kona mbalimbali nchini utasikia nyimbo zao zikisikilizwa;
10.JOEL LWAGA
Mwimbaji huyu wa Injili anafanya vizuri kwenye ulimwengu huo ambapo wimbo wake wa Sitabaki Nilivyo umekuwa gumzo kila kona ukisikilizwa na rika zote kuanzia watoto hadi watu wazima. Licha ya kwamba baada ya wimbo huo ametoa nyingine, lakini hazijatikisa kwani zimepokelewa na mashabiki wake kawaida tu na siyo kwa msisimko kama huo wa kwanza.
9.ANISETI BUTATI
Ni kijana ambaye ameibuka ghafla na kasi yake kuwa kubwa na ya aina yake kwani kwa kutoa tu wimbo wa kwanza umepokelewa vizuri na wapenzi wa Injili. Aniseti anatamba na Wimbo wa Wataulizana ambao ukipigwa hata kama umelala unajikuta unanyanyuka au kama unafanya kazi unabaki unatikisa kichwa tu kutokana na burudani yake.
8.CHRISTOPHER MWAHANGILA
Kwa sasa huyu jamaa anafanya vizuri na nyimbo zake ambapo wimbo unaojulikana zaidi ni ule wa Mungu Hawezi Kukusahau.
Mwanamuziki huyu tofauti na wimbo huo anafanya vizuri hata kwa nyimbo nyingine alizotoa kama Mungu ni Mungu, Yesu Yuko Hapa, Farao na nyinginezo.
7.WILLIAM YILIMA
Mtumishi huyu wa Mungu anatikisa na nyimbo zake nyingi na zote ni nzuri ambazo ziko kwenye albam inayokwenda kwa jina la Uko Wapi Mungu. Ukisikiliza nyimbo hizi hata kama una moyo mgumu kiasi gani, lazima utabadilika na kumrudia Mungu kwa kutubu maovu yako yote uliyoyatenda maana nyingi ni za kujutia.
6.ANGEL BERNARD
Ni mwimbaji wa kike ambaye anatikisa kwenye Injili kwa sasa. Wimbo wake maarufu ni ule wa Siteketei. Mwanamama huyu ambaye makazi yake ni mkoani Arusha amefanya pia kolabo na msanii maarufu wa Injili nchini Kenya, Mercy Masika unaojulikana kwa jina la Huyu Yesu.
5.SIFAEL MWABUKA
Heri Lawama ni wimbo ambao kijana huyu anaelezea mkasa wa kuacha uchawi na kuamua kuokoka ambapo watu wengi kutokana na wimbo huo wamekuwa wakihisi kuwa alikuwa mchawi kweli, lakini aliamua tu kuwaelimisha watu wa Mungu kupitia ujumbe huo.
Mwabuka anatikisa na wimbo huo pamoja na nyingine kama Umenipendelea, Usiogope Maneno Yao, Mimi ni Nani Baba, Shuka Tukuone Mungu Wetu na nyingine kibao.
4.MBARIKIWA MWAKIPESILE
Dhambi inaua…dhambi inaua…inaua vijana, watoto… ndiyo wimbo anaotikisa nao mwimbaji ambaye pia ni mchungaji. Albam hiyo ambayo imebebwa na jina la Dhambi Inaua ina nyimbo kali nyingi zikiwemo; Kazi Yangu Ikiisha, Sitanyamaza na nyinginezo.
3.BEATRICE MWAIPAJA
Huyu ni mdogo wa mwimbaji maarufu wa Injili, Martha Mwaipaja. Mwimbaji Beatrice anatikisa na nyimbo kama Kumbe ni Kwa Neema Tu na Mungu Umenihurumia.
2.CHRISTINA SHUSHO
Mkongwe wa Injili Christina aliyetikisa na ngoma kama Roho, Akutendee Nini na nyingine nyingi ameingia kwenye hii listi kutokana na kwa sasa anatamba na wimbo wa Relax. Mwanamama huyu mwenye sauti nzuri huwa hakosei kwani kila wimbo anaotoa unagusa mioyo ya wengi na kutikisa kila kona.
1.GOODLUCK GOZBERT
Huwezi kushindana…kushindana… na mwanadamu mwenye kinywa… ahayayaya… Hicho ni kipande cha wimbo wake alioutoa hivi karibuni unaojulikana kwa jina la Huwezi Kushindana. Kijana huyu mwenye sauti ya aina yake amekuwa akifanya vizuri kwenye ulimwengu wa muziki wa Injili na nyimbo zake nyingine kama Ipo Siku, Acha Waambiane na nyingine kibao.
SIGNATURE
Tags