Wanafunzi 1,222 waliofaulu wapewa zawadi na CCM


Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amesema kuwa ustawi wa elimu nchini umetokana na matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964.

Naibu huyo ameyasema hayo katika hafla ya kuwapatia zawadi Wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2018 waliofaulu kiwango daraja la I,II kwa shule mbali mbali za Zanzibar, hafla iliyofanyika katika kiwanja cha Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Unguja.

Dk.Mabodi amesema baada ya kufanyika Mapinduzi ya Zanzibar serikali ya wakati huo ikatangaza kuwa suala la elimu ni bure sambamba na kuimarisha miundombinu ya upatikanaji wa elimu kwa wananchi wote bila ubaguzi.

Amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuenzi Tunu ya Mapinduzi kutokana na mambo mema yaliyotekelezwa kwa haraka mara baada ya kufanyika mapinduzi hayo na wananchi wakapata uhuru na kunufaika na fursa ya elimu iliyotolewa kwa ubaguzi kabla ya mapinduzi.

Ameeleza kuwa kwa sasa Zanzibar imekuwa ni kitovu cha wasomi na watu wenye taaluma mbali mbali ambao chanzo cha mafanikio hayo kimetokana na kukua kwa sekta ya elimu nchini.

Jumla ya wanafunzi 1,222 waliofaulu mitihani ya kidato cha nne kwa kiwango cha daraja la kwanza na la pili(I,II) wamepatiwa zawadi mbali mbali na Chama Cha Mapinduzi ikiwa ni sehemu ya kuwapongeza na kuwahamasisha waendelee kusoma kwa bidii na kufaulu katika ngazi mbali mbali hadi Vyuo vikuu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad