JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro jana Ijumaa lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Majengo baada ya kugoma kuingia madarasani kwa kile walichodai ni kudhalilishwa kingono na kuchaniwa nguo na walimu wao.
Hatua hiyo imekuja mara baada ya wanafunzi hao kugoma kuingia darasani, kukataa kula chakula na kukusanyika mbele ya Ofisi ya Mkuu wa Shule hiyo huku wakitaka uongozi wa shule kufanya utatuzi wa sakata hilo.
Baadhi ya wanafunzi hao wamesema wamechoshwa na vitendo hivyo vya kikatili na udhalilishwaji wa kingono huko wakilitaka Jimbo Katoliki la Moshi na Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako kuingilia kati.
Kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Shule hiyo Gasto Lucas, amesema kuwa vitendo hivyo wanavyofanyiwa ni vya kudhalilisha utu wao kinyume na taratibu za nchi na wanapoulizia inakuwaje vitendo hivyo vinafanyika wanapigwa.
Kwa upande wake mwanafunzi Anithe Asenga amesema walimu wamekuwa wakiwanyanyasa wanafunzi wa kike na kuwadhalilisha huku wakichawachania sketi zao mbele na sehemu za kwenye mapaja.
“Tangu tumefungua shule hii ni sketi ya tatu nachaniwa tu jamani na sketi nimeshoneshewa hapa hapa shuleni, nimelipia Tsh. 20000 kwa kila sketi, “alisema.
Aidha akizungumza kwa niaba ya uongozi wa shule ya sekondari Majengo Mwalimu Mukindia Stephen amesema kuandamana siyo suluhisho hivyo aliwataka wanafunzi hao watawanyike warudi majumbani na uongozi wa shule utakaa na uongozi wa serikali ya wanafunzi kuzungumzia suala hilo.
Wanafunzi Waandamana Wakidai Kudhalilishwa Kingono na Walimu
0
February 09, 2019
Tags