Wananchi Waangusha Maombi Kwaajili ya Mauaji Njombe

Wananchi Waangusha Maombi Kwaajili ya Mauaji Njombe
MKUU wa Wilaya ya Njombe Ruth Msafiri (pichani) jana ameshiriki katika ibada ya kuhitimisha mfungo na Maombi yakuombea mkoa wa Njombe yaliyofanyika kwa wiki moja katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God T.A.G lililopo mtaa wa Melinze halmashauri ya mji wa Njombe mkoani humo.



Akiwa katika ibada hiyo,Msafiri aliwataka wakristo mkoani Njombe kuendelea kuombea mkoa wa Njombe kutokana na matatizo ya mauaji ya watoto yaliyojitokeza hivi karibuni huku akiwataka kuto kusahau kuombea maswala ya uchumi na familia kwa ujumla.



“Naendelea kuwategemea sana watu wa Mungu hatutafika bila kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja,kama tumeagiza kwa lazima kila mzazi awe na mtoto kila wakati ni lazima uchumi utashuka niwaambie kitu ambacho hamjajua halmashauri ya mji wa Njombe ni halmashauri ya kwanza Tanzania kwenye kipato cha juu kuliko halmashauri yeyote.



“Mwananchi wa Njombe wa kawaida tu kipato chake hakipungui milioni tano kwa mwaka hii ipo Njombe mji tu kwa Tanzania,sasa haya mambo mabaya yanatokea ili tupigwe katika uchumi wetu ni lazima tuungane katika hili na tunataka taifa hili liinuliwe kupitia Njombe”alisema Msafiri.



Aidha Msafiri alisema kuwa Serikali inaunga mkono jitihada hizo za kuuombea Mkoa huku akisema kuwa Serikali haijafurahishwa na mauaji hayo hivyo ni Wakati wa Kanisa Kuomba Zaidi Ili Matendo hayo yapotee kabisa Mkoani humo.



Naye mchungaji wa kanisa hilo Sefania Tweve alisema kuwa walikuwa na kazi kubwa ya kumlilia Mungu na kuombea mkoa wa Njombe,kuliombea Taifa,kuombea uchumi, kuombea ndoa pamoja na kushusha nguvu za giza kutokana na mambo maovu na ya kikatili yaliyotokea mkoani humo.



“Kwa kweli Taifa limetikisika sio siri tena ndio maana tumeingia kwenye maombi mazito tukianza na toba kwetu wenyewe kwamba Mungu atusamehe atupe njia iliyonyooka inawezekana kabisa sisi tulikosea na kujisahau sehemu ndio maana haya yote yakatokea na tunaamini kupitia maombi haya hakuna jambo litakalotokea tena”alisema mchungaji Tweve.



Waumini wa kanisa pia Walisema kuwa wakiwa kama wazazi Wanaolea Watoto Wadogo wanafahamu Uchungu wa kuondokewa na Watoto na Hivyo wanaamini Maombi hayo ya Siku Saba yameiweka Njombe Salama.



Hata hivyo timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) iliyoongozwa na Bi. Hanifa Selengu iliyofika mkoani Njombe kwa lengo la kuunganisha nguvu na Serikali ya Mkoa katika kupata namna bora ya kukomesha mauaji ya watoto yaliyotokea mkoani Njombe,nayo pia ilishiriki katika ibada hiyo ambapo mwenyekiti wa timu hiyo Hanifa Selengu akiwataka waumini hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ili kutokomeza mauaji hayo.



Jumla ya watoto saba mpaka sasa walifariki dunia kutokana na mauaji hayo huku mtoto mwingine aliyekatwa koromeo wiki chache zilizopita na kunusurika kifo,amefariki dunia na kufikia idadi ya watoto nane waliofariki kwa mauaji hayo huku watu 30 wakishikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano huku kesi zilizokamilia kuanza kufikishwa mahakamani Jumatatu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad