Waziri Mkuu Majaliwa Atoa Ufafanuzi 'sintofahamu' ya wakulima bei ya korosho

Waziri Mkuu Majaliwa Atoa Ufafanuzi 'sintofahamu' ya wakulima bei ya korosho
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa kuwalipa wakulima Sh2,600 kwa kila kilo moja ya korosho badala ya Sh3,300 kama ambavyo Serikali ilitangaza wakati wa mchakato wa kuzinunua mwaka jana.

Majaliwa ametoa ufafanuzi huo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la papo kwa papo aliloulizwa na mbunge wa Liwale (CCM), Zubery  Kuchauka.

Katika swali lake, Kuchauka amesema wakulima walio wengi  bado hawajapata fedha zao wakati Serikali imeshachukua korosho zao huku baadhi wakilipwa kidogo na  wengine wakilipwa Sh2,600  badala ya Sh 3,300 kama ilivyotangazwa na Rais John Magufuli.

Katika maelezo yake, Majaliwa amesema tamko la Rais Magufuli kununua korosho kwa Sh3,300 kwa kilo moja linahusu korosho daraja la kwanza na bodi ya zao hilo  ina sheria inayoeleza madaraja yalivyo.

“Kuna sheria inayoeleza korosho za daraja la pili zitauzwa kwa bei ya asilimia 80 ya daraja la kwanza. Ile ya Sh2,600 ni mahesabu yamefanyika ya asilimia 80 ya bei ya korosho daraja la kwanza na malipo yanaendelea vizuri.”

“Nataka niwahakikishie malipo yanaendelea na sehemu kubwa ya wakulima wamelipwa hasa wale chini ya kilo 1,500. Malipo yanayokuja sasa hivi ni zaidi ya kilo 1,500 na uhakiki umeshafanyika na taratibu wa kulipa unaendelea na utawafanya wakulima wapate fedha zao,” amesema.

Amesema korosho hazijakosa soko bali zimekosa bei nzuri ya kununuliwa ndiyo maana Serikali iliamua kuingilia kati na kuzinunua kwa wakulima ili wasipate hasara.

Majaliwa amesema wanunuzi wa zao hilo walikuwa wakinunua korosho kwa bei ya chini kuliko ile ya dunia jambo ambalo lilikuwa halimpi faida mkulima.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad