Waziri wa fedha wa zamani kutoa ushahidi kesi ya Kitilya

Waziri wa fedha wa zamani kutoa ushahidi kesi ya Kitilya
Waziri wa zamani wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, ameitwa kutoa ushahidi dhidi ya Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, na wenzake wanne.

Kitilya na wenzake hao wanakabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi pamoja na mashtaka 58 ya kula njama, kutakatisha fedha na kuisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani milioni sita.

Mbali na Kitilya, washtakiwa wengine ni Miss Tanzania wa 1996, Shose Sinare, Sioi Solomon, aliyekuwa Kamishna wa Sera na Madeni kutoka Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda (kwa sasa Ofisi ya Waziri Mkuu) na Alfred Misana, aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Sera na Madeni kutoka wizara hiyo (kwa sasa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto).

Wote kwa pamoja wanakabiliwa na tuhuma ya uhujumu uchumi iliyopewa usajili namba 2/2019.

Licha ya waziri huyo wa zamani mbali na Mkulo, shahidi mwingine aliyetajwa mahakamani kwa upande wa Jamhuri ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Jaji (mstaafu) Frederick Werema.

Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri unatarajiwa kuwasilisha vielelezo 218 zikiwamo nyaraka za benki kesi itakapopangwa kuanza kusikilizwa ushahidi katika Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.

Madai hayo yalitolewa jana na jopo la mawakili wa Jamhuri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuongoza mtandao wa uhalifu, uliosababisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata hasara ya dola za Kimarekani milioni 600.

Jopo la Jamhuri liliongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Fredrick Manyanda, Tumaini Kweka na Mawakili wa Serikali, George Barasa, Ester Martin na Leonard Swai.

Akiongoza jopo la mawakili wa serikali, Kweka alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), amewasilisha taarifa na kutoa kibali kwa Mahakama ya Uhujumu Uchumi kusikilizwa kesi hiyo.

Jopo la utetezi liliongozwa na Mawali Cathbert Tenga, Majura Magafu na Alex Mgongolwa.

Katika Kesi ya msingi washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 49 ya utakatishaji fedha, mashtaka matatu ya kughushi, moja la kuongoza mtandao wa uhalifu, mawili ya kutoa nyaraka za uongo, shtaka moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanyanyifu, kula njama ya kutenda kosa kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi (wakati huo ikijulikana hivyo, sasa Wizara ya Fedha na Mipango).

Upande wa Jamhuri ulidai katika shtaka la kwanza, ambalo ni la kuongoza mtandao wa uhalifu, washtakiwa kwa pamoja walitenda kosa hilo kati ya Februari 20, 2012 na Juni, 2015, katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam. Ilidaiwa kuwa kwa makusudi, washtakiwa waliongoza mtandao wa uhalifu, uliosababisha serikali kupata hasara ya dola za Kimarekani milioni 600.

Katika shtaka la kujipati fedha kwa njia ya udanganyifu, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Machi 15, 2013 na Januari 10, 2014, jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya, walijipatia Dola za Kimarekani milioni sita wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa malipo ya ada ya uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma (T) Ltd.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, ilidaiwa kuwa washtakiwa wote Machi 18, 2013 na Januari 10, 2014, jijini Dar es Salaam, walitakatisha Dola za Marekani milioni sita kwa kuzitoa fedha zilizoko katika akaunti ya Egma (T) Ltd iliyoko katika benki ya Stanbic Tanzania.

Aidha, katika shtaka la kuisababisha hasara serikali, ilidaiwa kuwa kati ya Mei Mosi, 2012 na Juni Mosi, 2015 jijini Dar Es Salaam, washtakiwa waliongeza gharama ya mkopo wa Dola milioni 600 kutoka asilimia 1.4 hadi asilimia 2.4, hivyo kuisababishia serikali hasara ya dola milioni sita.

Pia Sinare anadaiwa kuwa Agosti 2, 2012, akiwa na nia ya kudanganya, aliandaa nyaraka ya pendekezo la kifedha, akijaribu kuonyesha kuwa Benki ya Standard ya Uingireza ikishirikiana na Stanbic ya Tanzania watatoa mkopo wa Dola milioni 550 kwa serikali ya Tanzania kama ada ya uwezeshaji wa asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo huo wakati akijua kuwa si kweli.

Kwa upande wao, Shallanda na Misana, wanadaiwa kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri wao na tukio hilo wanadaiwa kutenda kati ya Septemba 11, 2012 na Oktoba 3, 2012 katika Wizara ya Fedha.

Katika kufanya hivyo, wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi wakionyesha nyaraka za pendekeo la kifedha la mkopo huo limetolewa Agosti 2, 2012 wakati wakijua ni uongo.

Mapema Aprili 2016, Kitilya, Sinare na Solomon, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka ya kula njama, kughushi na kutakatisha fedha.

Jana washtakiwa walipokumbushwa mashtaka yao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad