Waziri Wa Kilimo Abainisha Jitihada Za Serrikali Kwenye Mapinduzi Ya Kilimo Nchini

Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dr. John Pombe Joseph Magufuli, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuweka mazingira bora ya kuleta mapinduzi katika kilimo.

Japokuwa Kilimo kinachangia karibu asilimia 30 ya Pato la Taifa, ukuaji wa Sekta ya Kilimo bado hauridhishi kutokana na changamoto zilizopo, japo kumekuwepo na mwelekeo chanya katika siku za karibuni. Kulingana na taarifa zilizopo za hivi karibuni ukuaji wa sekta ya kilimo umefikia asilimia 7.1

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo jana tarehe 21 Februari 2019 wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa asasi zinazotoa huduma ndogo za fedha vijijini kwa Wajasiriamali Wadogo (TAMFI) katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania – Dar es salaam.

Alisema kuwa kwa kutambua hilo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo (ASLMs) kwa kushirikiana na wadau wa sekta inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme Phase Two-ASDPII).

Lengo kuu la ASDP II ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (mazao, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha na usalama wa chakula na lishe.

Alisema kuwa Utekelezaji wa lengo hilo ni kuhakikisha kuwa Taifa linaendelea kujitosheleza kwa chakula; kuimarisha uchumi; kuwa kichocheo cha kukua kwa viwanda; na kuongeza ajira. Ili kufikia malengo haya; Utekelezaji wa ASDP II utazingatia mnyororo wa thamani wa mazao ya kipaumbele ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Alizitaja jitihada zingine katika kuleta mapinduzi ya kilimo ambazo ni Kuanzishwa kwa eneo maalum la kuboresha mnyororo wa thamani kwa mazao mbalimbali (yaani The Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT), Kuanzishwa kwa Program ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (yaani Marketing Infrastructure, Value Addition and Rural Finance Support Programme –MIVARF) ambao lengo lake kuu ni kusaidia nyanja mbalimbali muhimu katika kuendeleza kilimo cha kisasa nchini na Kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo (yaani TADB) ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wakulima na shughuli za kilimo nchini.

Alisema kuwa Jitihada za dhati zinahitajika kuwashawishi vijana kwa njia mbalimbali ili nao waingie katika biashara ya kilimo hasa katika uboreshaji wa mnyororo wa thamani kutokea shambani hadi kwa mlaji.

Kuwepo kwa huduma kama bima ya afya kwa wakulima na makazi bora kunaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kuwafanya watu wengi zaidi haswa vijana kujihusisha na kilimo kwa njia za kisasa zaidi na usalama wa afya zao na makazi yao pia.

Allisema kuwa hiyo itakuwa njia bora ya kutatua mahitaji yao na kuwasaidia wakulima vijana kufanya shughuli za kilimo pamoja na kilimo biashara kwa ufanisi. “Umefika wakati sasa tuhamasishe kuwa na Kilimo cha mashamba makubwa na ya kati yatakayopelekea kuzalisha kwa wingi na kwa tija” Alikaririwa Mhe Hasunga

Mkutano huo utafanyika kwa siku mbili kuanzia leo tarehe 21 Februari 2019 mpaka kesho tarehe 22 Februari 2019 ukiwa na lengo la kujadili namna bora ya kuwajengea wakulima uwezo wa kustahimili matukio mbalimbali kwa kutumia huduma za fedha vijijini, namna ya kuwanufaisha wakulima na huduma za hifadhi ya jamii, bima ya afya, matumizi ya teknologia rafiki ya kuwafikishia huduma za fedha vijijini, makazi bora kwa wakulima pamoja na elimu ya fedha vijijini.

Mkutano huo umewajumuisha wadau mbalimbali wakiwemo maafisa kutoka serikalini, watoa huduma za kifedha vijijini, wataalam wa mambo ya kifedha, wakulima, na wawakilishi wa mashirika.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Ushauri kwa waziri wa kilimo na wadau wote. Nashukuru kwa yote myafanyayo. Ila tafadhali mapinduzi ya ya kilimo yasilenge ku eradicate organic food ambazo kwa kweli ni dhahabu na urithi was kipekee Mwenyezi Mungu aliowajalia binadamu hususan watanzania. Kwa afya bora za miili Yao with. Kamwe nisingependa tufikie mahalitambapo healthy and natural foods Zina geuka kuwa hadimu na ghali na ni matajiri tu ndo wenye uwezo wa kuvila. Future ya afya ya watanzania ipo mikononi mwenu kupitia maamuzi ya kimapinduzi ya kilimo mtakayoyafanya. Nawaombea hekima ya Mungu iwe nanyi. Fanyeni yote ila tuachieni natural food. Pia kilimo cha mkono kiwe mwisho. Halmashauri za wilaya zitoe huduma za matrekta kwa wakulima kwa bei nafuu. Kilimo cha umwagiliaji kiwe kipaumbele na mkulima wa kawaida awezeshwe kuwa na kilimo cha umwagiliaji.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad