Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi. SARAH COOKE, jana tarehe 4 Januari 2019 amemtembelea Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga na kufanya nae mazungumzo yenye lengo la kuongeza na kuimarisha Ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Uingereza katika sekta ya kilimo.
Katika mazungumzo hao, Mhe Hasunga na Bi. COOKE wamekubaliana kuongeza kasi ya Ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, makubaliano ambayo yatasaidia uwezekano wa kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kwa nchi zote mbili.
Katika kikao kazi hicho Waziri Hasunga amemueleza Balozi huyo kuwa serikali ya Tanzania imeanza zoezi la utambuzi wa wakulima nchini kwa kuwaandikisha ambapo mpaka sasa wakulima wa zao la Tumbaku wamekwisha andikishwa.
Hasunga alisema kuwa lengo la zoezi hilo la uandikishaji ni kuimarisha utambuzi wa wakulima ili serikali iweze kuwahudumia kwa weledi wakulima kote nchini kupitia pembejeo mbalimbali za kilimo ili kuondokana na wakulima hewa ambao wanatumia mwanya huo kuiibia serikali.
Vilevile amemueleza Balozi huyo kuwa serikali imejipanga kuimarisha sekta ya utafiti wa kilimo nchini jambo litakaloongeza tija na manufaa makubwa kwa wakulima nchini.
Katika mazungumzo hayo, Mhe Hasunga amemueleza Bi COOKE namna ambavyo serikali ya Tanzania imejipanga kuimarisha masoko ya ndani na nje ya nchi kwa wakulima.
Bi. COOKE, kwa upande wake amefurahishwa na jinsi ambavyo Waziri wa Kilimo pamoja na wasaidizi wake wanapambana kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli katika kuimarisha sekta ya kilimo sambamba na kuboresha masoko ya wakulima nchini.
Balozi huyo amemueleza waziri wa kilimo kuwa Uingereza itaendeleza maradufu ushirikiano na Tanzania kwani ni nchi yenye Amani na utulivu mwingi kwa wananchi wake.
Waziri Wa Kilimo Akutana Na Balozi Wa Uingereza Nchini
0
February 05, 2019
Tags