Agizo la Rais Magufuli Lasaidia Kuwatoa Kifungoni Wananchi Waliobambikwa Kesi Ya Mauaji Na Polisi



Na.Alex Sonna,Dodoma
BARUA ya wazi aliyoandikiwa Rais Dk. John Magufuli kupitia gazetini na mwananchi aliyebambikiziwa kesi ya mauaji imewezesha kuachiwa huru kwa mwananchi huyo huku Rais akiagiza hatua zaidi zichukuliwe kwa waliohusika kwenye tukio hilo linaloichafua serikali.

Mwananchi huyo Mussa Sadiki, aliandika barua ya wazi kwa rais Machi sita mwaka huu, akilalamikia kubambikiziwa kesi ya mauaji namba 8/2018 katika Mahakama ya Tabora baada ya kukamatwa na polisi ambapo baada ya rais kuisoma aliiagiza Ofisi ya Mwendesha Mashataka Mkuu wa Serikali, kuchunguza kubaini ukweli.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Mwendesha Mashataka Mkuu wa Serikali (DPP), Biswalo Mganga, amesema kuwa  baada ya mwananchi huyo kukamatwa, polisi walimnyang’anya sh. 778,000, simu ya mkononi na mali alizokuwa amenunua kwa ajili ya wakulima wakati akienda kwenye manunuzi.

“Kwa mujibu ya malalamiko yake aliyoyaandika gazetini, baada ya kukamatwa aliwekwa kwenye Kituo cha Polisi Tabora Mjini na kubambikizwa kesi ya kuvunja na kuiba ambapo alikaa kituoni kwa muda wa juma moja na alipopelekwa mahakamani alisomewa shtaka la mauaji,” alieleza.

DPP amefafanua  kuwa, baada ya Rais Dk. Magufuli kusoma barua hiyo, aliagiza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ifuatilie malalamiko ya mwananchi huyo haraka ili kujua ukweli.

Aidha amesema kuwa Ofisi ya DPP ilifuatilia suala hilo kwa kufanya mahojiano na mlalamikaji pamoja na kupitia nyaraka zilizopo katika kituo cha Polisi Tabora Mjini zinazohusiana na sakata hilo.

“Katika kufuatilia malalamiko hayo, ofisi ya DPP imebaini malalamiko hayo ni ya kweli. Hii ni kwa sababu kitabu cha kuzuia wahalifu (detention register) kilichopo katika kituo hicho cha polisi, kinaonyesha kuwa mwananchi huyo alikamatwa Juni 21 mwaka jana kwa kosa la kuvunja nyumba usiku na kuiba na aliingizwa mahabusu ya polisi saa tisa alasiri.

Hata hivyo amaesema kuwa  kitabu hicho kinaonyesha kuwa Juni 29 mwaka jana, mlalamikaji alitolewa mahabusu saa mbili asubuhi na kupelekwa mahakamani.

Mwendesha Mashtaka Mkuu  ameeleza alieleza kuwa, tarehe hiyo hiyo mwananchi huyo alifunguliwa kesi ya mauaji namba 8/2018 ikionyesha Mei sita mwaka jana katika barabara ya Kazima Tabora Mjini, alimuua Jackson Thomas.

Ameeleza  kuwa wakati wa kufuatilia malalamiko hayo, ofisi ya DPP ilibaini Julai mosi mwaka jana, alikamatwa Edward Matiku kwa makosa ya kuvunja nyumba usiku na kuiba lakini Julai 16 mwaka jana, naye aliunganishwa katika shauri la mauaji namba 8/2018 kuhusika na mauaji ya Jackson Thomas.

“Baada ya kuyabaini hayo, Machi nane mwaka huu, niliwafutia washtakiwa wote wawili mashtaka hayo na mahakama ikawaachia huru.

DPP  ameeleza kuwa baada ya Rais Dk. Magufuli kupokea ukweli wa malalamiko hayo na hatua zilizochukuliwa, anampongeza Mussa Sadiki kwa ujasiri aliouonyesha kwa kuweka wazi malalamiko yake.

Aidha amesema kuwa Rais anavishauri vyombo vingine vya habari kuchunguza na kuchapisha habari zenye ukweli kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

“Mheshimiwa Rais ameagiza hatua zaidi zichukuliwe kwa wote waliohusika na tukio hilo kwa lengo la kukomesha tabia kama hizo zinazoichafua serikali kwa wananchi wake na dunia nzima,” amesisitiza
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad