Kufuatia Simba kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa JS Saoura hapo jana nchini Algeria, Afisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara amezungumzia hatma yao katika michuano hiyo.
Muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo, Manara aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram akisema kuwa kwao mapambano bado yanaendelea na wanayo nafasi kubwa ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa ya vilabu barani Afrika.
"Ni Do or Die Match. Ni zaidi ya kufa au kupona Kwenye mchezo wetu wa mwisho dhidi ya AS Vita utakaochezwa Taifa, Jumamosi ijayo!!, bila kujali matokeo yatakayotokea Egypt baina ya Al Ahly na Soura ambao nao wanacheza siku hyo ya tarehe 16", amesema Manara.
"Ushindi wowote tutakaoupata dhidi ya Wacongo hao tutafuzu katika robo fainali!!. Hiyo sio 'Yes We Can', hiyo ni 'Do or Die' kama ilivyokuwa na Nkana, Insha'Allah itakuwa", amemalizia Manara katika ujumbe huo.
Kabla ya mchezo wa Simba hapo jana, ulitanguliwa na mchezo wa AS Vita Club walioikaribisha Al Ahly mjini Kinshasa, ambapo mchezo huo ulimalizika kwa AS Vita kuibuka na ushindi wa bao 1-0, bao lililofungwa katika na Tuisila Kisinda katika dakika ya 84'.
Baada ya matokeo ya michezo hiyo, sasa kundi D linaongozwa na JS Saoura yenye pointi 8 ikifuatiwa na Al Ahly na AS Vita Club zenye pointi 7 huku Simba ikiwa mkiani kwa pointi 6. Mpaka sasa timu yoyote katika kundi hilo inaweza kufuzu hatua inayofuata ya robo fainali endapo itashinda katika mchezo wa mwisho.
Hata hivyo baada ya kumalizika kwa mchezo wa JS Saoura na Simba, mashabiki na wadau wa soka nchini Tanzania wameonesha kutoridhishwa na kiwango cha beki, Paul Bukaba kutokana na kufanya makosa kadhaa ambayo yalipelekea kuadhibiwa kwa mkwaju wa penalti.