Baba Daimond: Kwa Mateso Haya Ninayoyapata Bora Nife tu

Baba Daimond: Kwa Mateso Haya Ninayoyapata Bora Nife tu
NI bora nife tu kwa mateso haya! Baba mzazi wa mwanamuziki kiwango wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Abdul Jumaa ‘Baba D’, amenyanyua kinywa chake kwa mara nyingine, Gazeti la Ijumaa lina habari ya kusikitisha.



Baba Diamond amesema kuwa, kwa mateso anayopitia anaona kifo ni halali yake na yuko tayari kutangulia mbele za haki. Baba D alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika mahojiano maalum aliyoyafanya na Gazeti la Ijumaa, nyumbani kwake, Magomeni-Kagera jijini Dar wakati gazeti hili lilipokuwa limekwenda kumjulia hali na kutaka kujua maendeleo ya afya yake.



Ikumbukwe kuwa, kabla ya hapo Baba D alilalamika kuwa hali yake ni mbaya baada ya kubainika kuwa na kansa ya ngozi na miguu yake kuharibika na kuvimba.

HUYU HAPA BABA D…

“Kwa kweli kuna wakati mtu unafikia unakata tamaa hadi unaona ni bora ufe tu maana hamna namna, miguu huwa inauma sana kwa kweli ni mateso kwelikweli,” alisema Baba D.



AMSHUKURU ZUBEDA

Alisema hata hivyo, anamshukuru Mungu baada ya mwanaye wa hiyari aitwaye Zubeda kujitokeza na kumsaidia matibabu ya awali ambayo yamemfanya angalau apate matumaini ya kuishi. Alisema tangu Zubeda alipofika akitokea nchini Uingereza hadi alipoondoka mapema wiki hii, angalau amerudisha matumaini japo bado hajapata tiba sahihi ya miguu hiyo ambayo ina vishiria vya ugonjwa wa kansa.



“Niliugua sana pale katikati, yaani kwa kweli hadi hivi tunaongea hapa ninamshukuru tu Mungu kwamba bado ninapumua. “Yule mwanangu (Zubeda) amenisaidia sana kabla hajaondoka, sasa kila siku zinavyozidi kwenda, hali inazidi kuwa mbaya,” alisema Baba D akitia huruma.


JITIHADA HAZIKUZAA MATUNDA

Alipoulizwa kuhusu jitihada zake za mwanaye huyo wa Uingereza kutaka kumsaidia kumkutanisha na familia ya mwanaye kwa maana ya mama Diamond (Sanura Kassim) na Diamond mwenyewe, alisema hazikuzaa matunda hadi alipoondoka mapema wiki hii.



“Aliniambia tu kwamba waliwasiliana na mama Diamond ambaye alimwambia kwamba atakuwa tayari kumsaidia tu pindi mwanangu yule atakapoanzisha matibabu kamili. “Lakini jitihada zake za kutukutanisha hazikuzaa matunda hadi alipoondoka na hata hivyo, sioni dalili zozote za kusaidiwa, ninamshukuru hata hivyo, ametumia fedha nyingi sana katika matibabu haya ya awali,” alisema mzazi huyo wa Diamond ambaye ni staa mkubwa Afrika Mashariki na Kati.



AMPA DIAMOND SIKU 7

Gazeti la Ijumaa lilimuuliza kuhusu habari iliyoandikwa na gazeti pacha la hili, Ijumaa Wikienda juu ya tatizo lake la miguu wiki mbili zilizopita kama ilimsaidia ambapo mzee huyo alisema hakupata msaada wowote kutoka kwa Diamond wala mama yake na kuamua kujipanga kuitisha mkutano mkubwa wa vyombo vya habari kama hatapata msaada.



“Kuna baadhi ya watu kutoka nje wameahidi kunisaidia akiwemo yule mwanangu (Zubeda) aliyeondoka hivyo kama itashindikana hapo baada ya muda kama wa wiki moja (siku saba) hivi nitaitisha mkutano wa wanahabari, niwaoneshe live hili tatizo langu waweze kunisaidia hata kama ni kwa kutangaza akaunti namba pamoja na namba zangu za simu,” alisema baba Diamond.


AMLAUMU QUEEN DARLEEN

Kwa upande mwingine, baba Diamond alisema amesikitishwa na kauli aliyoitoa mwanaye mwingine ambaye naye ni msanii wa Bongo Fleva, Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’ hivi karibuni katika vyombo vya habari (sio Global) kwamba Zubeda hamtambui kama dada yake na wana agenda yao binafsi.



“Queen kanisikitisha sana anasema eti yule sijui siyo dada yake sijui tuna ajenda yetu, lakini mimi niseme tu yule ni mwanangu kama alivyo yeye. Amejitoa na anaendelea kujitoa kunisaidia,” alisema baba Diamond. Kwenye mahojiano hayo, Queen alisikika akisema kuwa wamekuwa wakimsaidia sana baba Diamond kifedha, lakini hata wamsaidieje bado hawezi kuacha kuomba msaada. Queen hakuainisha fedha hizo ni kiasi gani na kama zinatosha kumtibu baba yao tatizo hilo la miguu.



DIAMOND ANASEMAJE?

Gazeti la Ijumaa lilimvutia waya Diamond juzi, lakini kama ilivyo kawaida yake, simu yake iliita bila kupokelewa. Kwa nyakati tofauti gazeti hili limekuwa likimtafuta Diamond ili kuweza kusikia kauli yake kuhusu suala hilo la ugonjwa wa baba yake huku likimtumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS), lakini kama kawaida yake huwa hajibu chochote.



BABA D KUUMWA

Historia ya afya ya baba Diamond ilianza kuyumba tangu mwaka 2015 alipojitokeza kwenye vyombo vya habari na kueleza namna ambavyo miguu ilikuwa ikimtesa.

Mwaka 2016 alitoa kauli nzito akimuomba Diamond amsaidie matibabu la sivyo ikitokea akafa, basi asimzike. Kama hiyo haitoshi, baada ya hali yake kuendelea kuwa tete, mwaka alimuoba Diamond kama ameshindwa kumsaidia chochote basi amkatie hata bima ya afya alipokuwa akiwakatie mashabiki wake wa Tandale jijini Dar.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad