Msanii wa muziki nchini Uganda ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kyadondo, Bobi Wine amesema kuwa siku za Rais wa Taifa hilo, Yoweri Museveni za kukaa madarakani zinahesabika.
Bobi Wine
Bobi Wine akihutubia maelfu ya watu waliojitokeza katika ziara yake ya kutoa shukrani mjini Arua Jumapili iliyopita, amesema kuwa 2021 hana imani kama Museveni atasalia madarakani kwani amekuwa akiminya demokrasia hata ndani ya chama chake cha NRM, hivyo hawezi kushinda uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2021.
“Nakwambia (Rais Museveni) siku zako za kukaa madarakani zinahesabika. Inaingiaje akilini kutwambia uliingia msituni kutafuta Demokrasia ile hali unashindwa hata kuonesha Demokrasia ndani ya chama chako cha NRM, Tena ukiwa tayari umefikisha miaka 33 madarakani,“. amesema Bobi Wine.
Ziara hiyo ya Bobi Wine, ililenga kuwapongeza wananchi wa jimbo la Arua kwa kumchagua Mbunge Kassiano Wadri ambaye alikuwa anampigia upatu kwenye kampeni za uchaguzi mwaka jana, kabla ya kukamatwa na kupigwa na jeshi la polisi kwa kuhusishwa na vurugu za kuzuia msafara wa Rais Museveni.
Kauli hiyo, inakuja ikiwa ni siku chache zimepita tangu chama cha NRM kumtangaza kuwa, Rais Museveni ndiye atakayegombea urais mwaka 2021 kupitia chama hicho tawala.
Rais Museveni baada ya kupitishwa na chama chake, alisikika akimuonya Bobi Wine kuwa ni vyema angeendelea kwenye muziki na aachane na siasa.
Bobi Wine amejibu kauli hiyo kwenye ziara hiyo kwa kusema “Wakati yeye alivyokuwa na umri kama wangu alikuwa mchungaji, kwanini hakuendelea kuchunga na akaamua kuingia kwenye siasa?, nawambieni tuitafanya kama tulivyofanya mwaka jana hapa Arua.“.
Bobi Wine amejipanga mwaka 2021 kugombea urais kama mgombea huru na tayari wanasiasa wengi wakongwe wamemtabiria kuwa atakuwa mpinzani mkubwa wa Rais Museveni.
Bobi Wine amtumia salamu za vitisho Rais Museveni ‘siku zako zinahesabika za kukaa madarakani’
0
March 26, 2019
Tags