ACHANA na Clatous Chama ambaye alifunga bao lililoipeleka Simba kwenye hatua ya makundi na vilevile akapachika lililoivusha robo fainali.
Kwenye Simba kafanya vizuri lakini Zambia timu yake ya Taifa imechemka. Wameenda kuishukia Namibia mabao kibao yote kazi bure.
Kuna mtu mmoja anaitwa John Bocco. Anastahili heshima ndani ya ardhi ya Tanzania, ameweka rekodi ambayo hata Chama imemshinda pamoja na mbwembwe zake zote.
Ameweka rekodi ya kipekee baada ya kuzisaidia timu mbili za Simba na Taifa Stars kufanya makubwa mwaka huu na kurejesha heshima ya Tanzania.
Bocco ambaye amefunga mabao tisa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, hadi sasa amehusika kwenye kutengeneza mabao matatu muhimu kuliko wachezaji wengine wote wa Tanzania.
Bocco ambaye ni mchezaji wa zamani wa Azam, alianza kazi yake hiyo kwenye mchezo wa Simba dhidi ya AS Vita Club wa kutafuta nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo huo, Bocco ndiye alitoa pasi ya bao la ushindi kwa timu yake katika dakika ya tisini ambapo Simba ilipata ushindi wa mabao 2-1 na kwenda robo fainali.
Alipiga pasi ambayo ilirukwa na kiungo Haruna Niyonzima na mpira ukamfikia mfungaji Clatous Chama ambaye aliifungia timu yake bao hilo muhimu na kuipeleka Simba kwenye robo fainali.
Hata hivyo, baada ya kumaliza kazi kwenye klabu yake, Bocco alifanya tena mambo makubwa kwenye mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Uganda ambapo aliipa timu hiyo ushindi tena kwa staili ileile.
Bocco alitoa pasi mbili za mabao kwenye mchezo huo ambao Taifa Stars walipata ushindi wa mabao 3-0.
Mshambuliaji huyo mwenye upeo wa kuchanganua mambo, alitoa pasi ya bao la kwanza na la mwisho, huku lile la pili likifungwa na beki Erasto Nyoni kwa mkwaju wa penalti baada ya mchezaji mmoja wa Uganda kuunawa mpira eneo la hatari.
Pasi hizo mbili ni zile za mabao ya Simon Msuva na Aggery Morris, yaliyoifanya Taifa Stars ifuzu Afcon ambapo fainali zake zinatarajiwa kufanyika nchini Misri kuanzia Juni mpaka Julai, mwaka huu.